Rais Kenyatta asikia kilio cha Wakenya kuhusu kodi ya bidhaa za mafuta

Hatimaye Rais Uhuru Kenyatta ametoa pendekezo kwa bunge kupunguza Kodi ya Thamani ya Ziada kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8. Akilihutubia taifa muda mfupi uliopita, Rais Kenyatta amesema ameitikia vilio vya wananchi, ndiposa amelirai bunge kuufanyia marekebisho Mswada wa Kifedha 2018, ili kujumuisha pendekezo lake. Iwapo bunge litazingatia, bei za mafuta zitashuka angaa kwa kiasi fulani.

Huku akikiri kwamba taifa linakabaliwa na matatizo mbalimbali za kifedha, Rais Kenyatta amependekeza njia nyingine za kupunguza matumizi ya fedha za serikali kukiwamo kupunguza safari za nje za maafisa wa umma, kupunguza mafunzo mbalimbali ya idara za serikali miongoni mwa mbinu nyingine.

Ili kuziba mianya ya wizi wa fedha za umma, Rais amependekeza kuongezwa kwa bajeti ya idara ya mahakama na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ili kuziwezesha kukamilisha kwa haraka kesi mbalimbali za ufisadi kwa lengo la kurejesha mali ya umma iliyotwaliwa.

Related Topics

Rais Kodi