Spika Justin Muturi akataa kuidhinisha orodha ya viongozi wa NASA bungeni
Na Carren Omae
Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi amekataa kuidhinisha orodha ya viongozi wa upinzani bungeni iliyowasilishwa katika bunge hilo. Muturi amesema utaratibu wa sheria za bunge haukufuatwa na upande wa wachache bungeni wakati wa uteuzi wa wawakilishi wao. Spika Muturi hata hivyo ameuagiza upinzani kuwasilisha upya orodha ya majina ya viongozi wake bungeni humo Novemba tarehe 7 wakati bunge litakaporejelea vikao.
Kadhalika hatua yake ya orodha hiyo ni kufuatia barua za malalamiko ambazo amepokea kutoka kwa vyama tanzu vya muungano wa NASA kuhusu uteuzi huo.
Kulingana na kifungo cha 20(4) cha sheria za bunge, ni Kiranja wa Wachache anayestahili kuwasilisha ujumbe kwa Spika kuhusu uteuzi wa viongozi wake bungeni. Hata hivyo Mbadi ameahidi kwamba upinzani utafuata sheria katika kuwasilisha orodha ya majina hayo.
Katika Orodha hiyo, NASA imempendekeza Mbunge wa Suba Kusini, John Mbadi wa ODM kuwa Kiongozi wa Wachache huku Naibu wake akiwa Mbunge wa Lugari, Ayub Savula wa Chama cha ANC.
Mbunge wa Kathiani, Robert Mbui wa Wiper alipendekezwa kushikilia wadhfa wa Kiranja huku Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa wa Ford - Kenya akipendekezwa kuwa Naibu wake.
Ikumbukwe hatua ya NASA kuchelewa kuwasilisha majina ya viongozi wake bungeni vilevile imechelewesha kubuniwa kwa kamati muhimu bungeni kama vile Kamati ya Haki na Sheria.
Ikumbukwe, Bunge la Kitaifa na Seneti limeanza likizo leo kupisha marudio ya uchaguzi wa urais?