Wabunge wateule walalamikia mishahara

Na, Beatrice Maganga
Wabunge wateule walalamikia mishahara
Mzozo umeanza kutokota baina ya wabunge wateule na Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma, SRC kufuatia hatua ya wabunge hao kuanza kulalamikia suala la kuondolewa kwa marupurupu yao. Wabunge hao wameitaja hatua hiyo kuwa kandamizi na ambayo huenda ikaathiri utendakazi wao na hata kulidunisha bunge.
Hata kabla ya kuapishwa rasmi kuanza kutekeleza majukumu yao, wabunge wateule wakiongozwa na Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Homabay, Gladys Wanga wamesema huenda wakageuka na kuwa ombaomba kufuatia kupunguzwa kwa mishahara na marupurupu yao waliyokuwa wakitegemea pakubwa kuendelezea shughuli zao.
Wanga amesema vigezo vilivyotumiwa na SRC inayoongozwa na Sarah Serem kuafikia uamuzi huo havijawekwa bayana wala tathmini ya utendakazi wao kukufanywa.
Aidha amesema huenda wabunge wakapitia changamoto za usafiri wanapoendeleza huduma zao iwapo watanyimwa fursa ya kupewa ruzuku ya kununua magari.
Ikumbukwe mnamo mwezi Juni mwaka huu, SRC ilitangaza hatua mbalimbali za kupunguza gharama za kulipia mishahara ya wafanyakazi wa umma. Njia mojawapo ilikuwa kupunguza mishahara ya Rais, Naibu, wake, magavana, wabunge na viongozi wengine wa kisiasa.
Kwa mujibu wa mwongozo wa SRC, mshahara wa Rais utapunguzwa kutoka shilingi milioni 1.6 kwa mwezi hadi takriban shilingi milioni 1.4, mawaziri shilingi takriban 924,000 kutoka zaidi ya shilingi milioni moja, huku wabunge wakilipishwa shilingi 621,000 kutoka 710,000. Marupurupu ya wabunge kuhudhuria vikao vya bunge vilevile yalipunguzwa.
Ilivyo sasa, wenyeviti wa kamati  mbambali za bunge hulipwa shilingi elfu kumi wanapoitisha kikao maalum huku wabunge wakilipwa shilingi elfu tano kwa kila kikao.
Bila shaka suala hili huenda likazua mijadala mikali baada ya wabunge kuapishwa wiki ijayo. Ikumbukwe Rais Uhuru Kenyatta aliunga mkono kupunguzwa kwa mishahara hiyo. Hata hivyo inasubiriwa kuona iwapo wabunge ambao sasa imebainika wengi ni wa Jubilee watazingatia uamuzi wa kiongozi wao ama watakaidi na kufanya mageuzi ya kujinufaisha kifedha. 

Related Topics