Nyong'o Azindua Rasmi kuwania Ugavana

Na Sophia Chinyezi
Seneta wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o amezindua rasmi azma yake ya kuwania ugavana katika kaunti hiyo. Akiwahutubia wanahabari mapema leo, Nyong’o aidha amemtangaza Mathews Owili kuwa mgombea mwenza wake. Owili ambaye ni mzaliwa wa eneo la Nyakacha amesema yuko tayari kwa kazi hiyo na kuahidi kwamba atatekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.
Ikumbukwe Nyong’o alitajwa kuwa mshindi wa uteuzi wa ODM mwezi uliopita baada ya kutofautiana na Gavana Jack Ranguma. Wote walikuwa wametangazwa washindi wakati huo.
Nyong’o alitangazwa kuwa mshindi na afisa aliyesimamia uchaguzi katika kaunti hiyo Tom Okong’o katika Shule ya Sekondari ya Thurdibuoro baada ya kupata kura 164,110 dhidi ya kura elfu 91, 480 alizopata Ranguma.
Katika ukumbi wa Aga Khan mjini Kisumu, Ranguma alitangazwa kuwa mshindi na naibu afisa msimamizi wa uteuzi huo Richard Kiyondi kwa kupata kura elfu 118,934 dhidi ya kura elfu 32,028 alizopata Nyong’o.
Baadaye mwenyekiti wa Bodi ya Uteuzi wa Chama hicho Judith Pareno alisema kuwa Nyong’o ndiye aliyeshinda kwa kura elfu 164,553 dhidi yakua wlfu 98,573 za Ranguma.