BARAZA LA MAGAVANA KUWALIPA MADAKTARI

Na Sophia Chinyezi

Magavana wametangaza kwamba kaunti zitawalipa madaktari mishahara ya siku mia moja ambazo walishiriki mgomo. Mwenyekiti anayeondoka wa Baraza la Magavana ambaye pia ni Gavana wa Meru Peter Munya mapema leo amesema uamuzi huo umeafikiwa kwa kuzingatia masuala mbalimbali ya kibinadamu. 
 
Akizungumza na wanahabari, Munya vile vile ametaja hatua zilizochukuliwa kuboresha huduma katika sekta ya afya. Ameongezea kuwa wameendelea kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuanzisha vituo zaidi vya afya na kusambaza dawa pamoja na vifaa vya matibabu. Kadhalika amesema wamehakikisha kuwa vituo hivyo vina wahudumu wa kutosha.
Magavana aidha wamehusisha upungufu wa mahindi nchini na ukosefu wa ushirikiano baina ya Serikali ya Kitaifa na Kaunti. Munya amesema serikali pamoja na kaunti zinastahili kuweka mikakati mwafaka ya jinsi ya kuiendeleza nchi, hasa uzalishaji wa bidhaa za kilimo.
Kwenye kikao hicho, Gavana wa Turkana Josephat Nanok ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana baada ya mihula miwili ya kuhudumu ya Munya kukamilika. Nanok ni Gavana wa tatu kushikilia wadhifa huo. Gavana wa Bomet Isaac Ruto ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza kushikilia wadhifa huo kutoka mwaka 2013 hadi Mei 21 mwaka 2015. ?