Mkutano wa 'Team Nairobi' watibuka

Na Rosa Agutu
NAIROBI, KENYA, Rabsha zimeshuhudiwa katika mkutano wa Jubilee uliokuwa ukiendalia katika Ukumbi wa Bomas, Kaunti ya Nairobi kufuatia mvutano kati ya wafuasi wa Seneta wa Nairobi, Mike Sonko na wa Mbunge wa Starehe Maina Kamanda, kuhusu usimamizi wa bodi ya uchaguzi wa Kaunti ya Nairobi.

Wafuasi wa Sonko waliondoka kwenye mkutano huo ghafla wakidai kuwa Kamanda alikuwa na njama ya kuiba kura hizo kwa kumpendelea Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth madai ambayo yanapingwa na Kamanda.

Haya yalijiri baada ya wawaniaji mbalimbali kutoa mapendekezo ya watu ambao wangewataka wasimamie uchaguzi huo. Msimamizi wa bodi hiyo Michael Waweru amelazimika kukatiza kikao hicho punde wafuasi wa viongozi hao walipoanza kuzua vurugu kwa kurushiana viti.

Awali, Margaret Wanjiru na Mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru wanaokimezea mate kiti cha ugavana Kaunti ya Nairobi pamoja na Sonko, walitarajiwa kuwasili mkutanoni kutoa tangazo muhimu linalohusiana na vuguvugu la Team Nairobi. Hata hivyo, ni Sonko na Wanjiru pekee waliokuwapo kwenye mkutano huo.

 

Related Topics