''Fedha za NYS hazitaibwa tena!'' Asema Ruto

Na Beatrice Maganga

''Wizi wa fedha za umma kupitia miradi ya Taasisi ya Kitaifa ya Huduma za Vijana, NYS hautashuhudiwa tena.'' Kauli hiyo imetolewa na Naibu wa Rais William Ruto ambaye amesema serikali imeweka mikakati kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma.

Ikumbukwe washukiwa kadhaa wamefikishwa mahakamani kwa madai ya kufuja kima cha shilingi milioni 791 kupitia miradi ya NYS.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua sera ya kitaifa ya kujitolea, yaani National Volunteer Policy kwenye Kaunti ya Garissa, Ruto aidha ametoa wito kwa vijana kusajiliwa kupewa vitambulisho vya kitaifa. Amesema stakabadhi hiyo muhimu itawasaidia vijana kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kwa upande wake Waziri wa Jinsia na Vijana, Cecily Kariuki amesema vijana watakaoshirikishwa katika miradi ya NYS watafunzwa namna ya kuwekeza fedha zao kwa siku za usoni.