Taharuki yatanda Narok kufuatia uvamizi

Na, Sophia Chinyezi

Familia sita zimeachwa bila makao kwenye Kaunti ya Narok baada ya watu wasiojulikana kuteketeza nyumba zao usiku wa kuamkia Jumanne. Takribani nyumba kumi zimeteketezwa wakati wa kisa hicho kilichotokea kwenye maeneo ya Pimbiniet na Olopirik mpakani pa Transmara Mashariki na Magharibi, mwendo wa saa tatu usiku na saa tano.
Inaarifiwa kisa hicho kilitokea kufuatia tofauti zilizoibuka kati ya jamii za Kipsigis na Maasai. Kwa mujibu wa wa OCPD wa Transmara, Ambrose Hongo, kisa hicho kilijiri wakati wenyeji walipokuwa wamelala na kusema maafisa wa usalama wanafanya uchunguzi kuwatambua wahusika.
Hata hivyo amesema kufikia sasa, hakuna aliyekamatwa akihusishwa na kisa hicho, ingawa polisi wameimarisha doria kwenye mpaka unaozitenganisha jamii hizo. Kisa hicho kinajiri wiki kadhaa baada ya kamati ya usalama eneo hilo kuwaonya wakazi dhidi ya kumiliki silaha hatari.