IEBC kubadili mtindo wa kutangaza matokeo ya uchaguzi

Na, Suleiman Yeri,
IEBC kubadili mtindo wa kutangaza matokeo ya uchaguzi
Tofauti na miaka ya awali ambapo matokeo ya kura ya urais yaliyowasilishwa Bomas yalitangazwa huku mengine yakisubiriwa, Tume ya Uchaguzi IEBC inasema wakati huu, mtindo tofauti utatumiwa.
Afisa mkuu mtendaji wa IEBC, Ezra Chilobah amesema badala ya kutoa matangazo ya mara kwa mara ya matokeo ya kura za urais yanayofika Bomas, tume hiyo sasa inasema haitatoa tangazo lolote bali itasubiri hadi ipokee na kujumlisha matokeo kutoka maeneo bunge yote 290 nchini, kisha kutoa tangazo kuhusu idadi jumla, vilevile mshindi wa kura ya urais.
Chilobah ameongeza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kuwa matokeo yatakayo tangazwa katika maeneo bunge ndiyo yatakayo kuwa rasmi na hivyo hawatakuwa na ulazima wakuyatangaza tena.
Wakati uo huo amesema kuwa Kituo cha kitaifa cha kukusanya matokeo ya uchaguzi katika Ukumbi wa Bomas kitakuwa tayari kufikia mwishoni mwa wiki hii.
Aidha hii ni mara ya pili kwa ukumbi huo wa tamasha za kitamaduni kutumika kuwa kituo cha kitaifa cha kukusanyia matokeo ya uchaguzi na ulifungwa kuanzia terehe 28 mwezi juni ili kutoa fursa kwa ujenzi wa matumizi ya Tume hiyo.

Related Topics