Rais akabidhiwa ripoti kuhusu ukame

Na Sophia Chinyezi
Rais Uhuru Kenyatta amekabidhiwa ripoti kuhusu hali ya ukame nchini na mikakati iliyowekwa na serikali kuu na washikadau wengine kukabili hali. Mawaziri na makatibu wa Wizara za Ugatuzi, Fedha, Kilimo, Leba na Masuala ya Afrika Mashariki, wamemueleza Rais kwamba kaunti ishirini na tatu zilizo katika maeneo ya jangwani zimeathirika pakubwa na ukame.
Hata hivyo wamesema mikakati mwafaka imewekwa kuhakikisha hakuna Mkenya atakakufa kutokana na njaa. Rais Kenyatta amesema atakutana na mawaziri hao tarehe 27 mwezi huu kupata ripoti kamili ya hali hiyo. Aidha ameongeza kuwa watatathmini bajeti kushughulikia tatizo hilo, huku akiziomba serikali za kaunti kubuni mikakati itakayosaidia kupata suluhu ya ukame.
Waziri wa Fedha Henry Rotich na mwenzake wa Ugatuzi Mwangi Kiunjuri wamemfahamisha Rais kuhusu uamuzi wao wa kuwashirikisha washikadau wengine ambao wako katika maeneo yaliyoathirika ili kutoa usaidizi unaohitajika.
Mawaziri hao vilevile wamesema serikali imekuwa ikisambaza chakula cha msaada kwa Wakenya milioni 1.5, wengi wakiwa wa maeneo ya jangwani.