×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jihadharini wenzangu, ulimi kiungo hatari

News

Vongozi wa dini wamekizungumzia, na wangali kukizungumzia. Binadamu anakihitaji sana kiungo hiki. Kiungo uhai. Kiungo kidogo tu. Katiti sana! Lakini kinaweza kufanya makubwa. Na madogo pia.

Si kingine ela ni ULIMI.

Kuleta utu ni ulimi, kurubuni ni hicho. Mwanzo wa ndoa – kutongoza – ni hicho. Yaani kwa kifupi ni kuwa maisha hayendi bila kiungo hiki.

Nchi nyingi, hasa bara la Afrika, zimesambaratika kutokana na ULIMI. Viongozi wengi, wameongoza na kutawala miaka na mikaka kutokana na "ukweli-urongo" wa ulimi.

Leo hii ukisikia machafuko katika nchi nyingi duniani, utesi wa kikabila, uadui wa dini, daawa ya mipaka, basi jua wazi kuwa aghalabu mizozo hii imesababishwa na ulimi. Aidha, ni ulimi uo huo ndio ambao kwamba hutumiwa kuleta amani katika jamii.

Ndio maana leo nauona ulimi kuwa chanzo cha utengano na mwisho wa utangamano.

Hivi hekaya zangu za leo zalenga nani na wepi? Njoo sasa nikupakulie.

Nchi hii ilikumbwa na zogo baya sana baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007. Mbali na mauaji, uharibifu wa mali na uhuni mwingineo dhidi ya binadamu, nchi hii ilijikuta katika madaftari ya mahakama ya kimatiafa ya jinai huko the Hague, Uholanzi, ICC.

Je, tulijifunza nini kutokana na uchochezi wa ndimi zetu wakati huo? Hivi huwa twajifunza nini kutokana na uchochezi wa ndimi pindi tukaribiapo uchaguzi? Mbona tunasahau ulimi na madhara yake katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda na kwingineko? Kwa nini siye tungali twatoroka na utumbo wa wenzetu kumbe kesho, nao wenzetu watakimbia na utumbo wetu?

Wapo wanasiasa nchini, magavana, maseneta, wabunge, mawaziri na wadau wengineo ndani na nje ya serikali (kwa maana ya upinzani) ambao ni 'wataalamu' wa matusi na uchochezi. Hawana kaba ya ulimi. Ndio ukaambiwa heri kujikwaa kidole kuliko ulimi. Hii sio mara ya kwanza sisi kuwaona wakifikishwa kizimbani kwa kutumia ndimi zao visivyo. Hivi tutawavumilia hadi?

Vyombo vya habari, mitandao ya kijamii ingali kurindima na kulaani vikali wanasiasa wachochezi, hasa kufuatia matamshi yaliyoishia kutiwa nguvini kwa seneta Johnstone Mutahama, wabunge Ferdinad Waititu, Kimani Ngunjiri, Moses Kuria, Junet Mohammed, Aisha Jumwa, Timothy Bosire na Florence Mutua. Matokeo yake je? Kuachiliwa kwa dhamana!

Siku ni za kuhesabu tu kabla ya kuandaliwa uchaguzi mkuu nchini Kenya mwakani. Na tayari wanasiasa wameanza kuzitumia ndimi zao vibaya. Twambiwa kuwa dalili ya mvua ni mawingi. Asiyejua kufa na atazame kaburi. Asiye na tahadhari ni ng'ombe!

Huu ndio wasaa wa serikali kuziba ufa kabla ya kujenga ukuta. Wizara ya usalama wa ndani mpo? Wakuu wa dola na taasisi za jeshi na polisi mpo? Tume ya Taifa ya Maridhiano na Utangamano ipo?

Hili domo kaya tunalopiga sasa litatumaliza jamani. Tutaangamia. Ni wajibu wangu na wewe kusema sasa kabla ya majuto ya mjukuu. Sema kitu. Tusema jambo jamani. Tusitahamaki asubuhi kutafuta blanketi wakati kumekwisha kupambazuka!

Ulimi uo huo twautumia sana vibaya kutusiana na kuchocheana katika mitandao ya kijamii. Si Twitter, si Facebook, si wepi vile.....

Lazima na sharuti hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wachochezi.

Ulimi jamani.

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).

[email protected], [email protected],

FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,

Twitter: @alikauleni

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles