Maafisa wakuu katika Wizara ya Afya watakiwa kujiuzulu kufuatia sakata ya shilingi bilioni tano

Na Carren Omae

Sakata nyingine kubwa kuhusu ufujaji wa pesa katika Wizara ya Afya ambayo imeibuka tayari imechochea hisia kali nchini. Huku uchunguzi kuhusu sakata hiyo ukiendelea, baadhi ya viongozi wametoa wito kwa maafisa wakuu katika wizara hiyo kujiuzulu ili kutoa nafasi ya uchunguzi huo kufanywa.
Alhamisi Waziri wa Afya Cleopa Mailu na Katibu wa Wizara hiyo, Nicholous Muragori walikosa kufika mbele ya Kamati ya Afya ya Seneti kujibu maswali yanayohusu sakata hiyo. Sababu walizotoa ni kwamba walikuwa katika mkutano mwingine kuhusu tatizo lilo hilo, vilevile kukusanya stakabadhi watakazoziwasilisha mbele ya kamati. Mwenyekiti wa kamati hiyo Wilfred Machage ameeleza kusikitishwa na hulka za maafisa wa umma kufuja fedha zinazotengewa miradi muhimu nchini.
Baadhi ya wanachama wa kamati hiyo wamesema maafisa hao pamoja na wengine wanaohusishwa wanafaa kuwajibika. Wanakamati hao akiwamo Seneta wa Wajir, Ahmed Abdulahi na Seneta Maalumu, Ziporah Kitony wamesema wanafaa kujiuzulu nyadhifa zao.
Mailu na Muragori wametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Jumanne wiki ijayo.
Sakata hiyo inayoashiria kupotea kwa zaidi ya shiingi bilioni tano, inadaiwa kuwahusisha maafisa wakuu wa Wizara ya Afya waliovuruga mfumo wa ki-dijitali wa malipo ya serikali, maarufu IFMIS na kutumiwa vibaya kwa mabilioni ya pesa zilizonuiwa kununua vifaa na kulipia huduma za matibabu.