Nafasi za makamishna wa IEBC zatangazwa kuwa wazi

Na Sophia Chinyezi

Jopo Maalum lililoteuliwa kushughulikia uteuzi wa Makamishna wapya wa Tume ya Uchaguzi, IEBC limetangaza nafasi hizo kuwa wazi. Walio na nia ya kuwania nafasi hizo wana hadi Novemba tarehe 7 kutuma maombi yao. Kwenye tangazo lililochapishwa katika gazeti za humu nchini, watakaotuma maombi kwa nafasi ya Mwenyekiti wanastahili kuwa na digrii kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na kuwa na tajriba katika masuala ya uchaguzi, usimamizi na uongozi. Tangazo hilo vilevile limetaja kuwa mgombeaji anastahili kuhitimu kushikilia ofisi ya Jaji wa Mahakama ya Juu. Aidha anatarajiwa kuwa na mahitaji yote yaliyoratibiwa katika sehemu ya sita ya katiba.
Mwenyekiti pamoja na makamishna wa tume hiyo watahudumu kwa muhula mmoja, ambayo ni miaka sita. Jopo hilo litaanza shughuli ya kuwateua makamishna hao wapya kuanzia katikati ya mwezi ujao. Baadaye wataendesha mahojiano kwa watakaoorodheshwa. Mahojiano hayo yatafanywa hadharani kati ya Novemba 22 hadi 26 mwaka huu.
Wanachama watawasilisha majina mawili kwa wadhifa wa Mwenyekiti na mengine tisa kwa wadhifa wa makamishna kwa Rais Uhuru Kenyatta. Rais atakuwa na siku saba kumteua Mwenyekiti na makamishna sita, kisha kuwasilisha orodha hiyo bungeni. Hata hivyo muda wa bunge kutathmini majina hayo haujatengwa, ingawa kuna mchakato wa kupunguza muda huo hadi wiki mbili. Baada ya kupokea ripoti ya Bunge, Rais atakuwa na siku saba zaidi kufanya uteuzi. Makamishna hao wapya wataapishwa muda mfupi baadaye.