Jaji Mbogholi ashindwa kuwatambua Magavana

Na, Beatrice Maganga/Mate Tongola

Shughuli ya kuwachuja wanaowania wadhifa wa Jaji Mkuu, imeingia siku ya pili leo hii huku Jaji Msagha Mbogholi akitathminiwa ili kujua iwapo anawafahamu baadhi ya viongozi wa kaunti. Mbogholi alitakiwa kuwataja baadhi ya viongozi wa kaunti, baada ya kuelezea imani aliyo nayo kuhusu mfumo wa ugatuzi, suala lililompiga chenga.
Jaji Mbogholi aidha alitakiwa kuelekeza sababu za kutojiunga na mitandao ya jamii kama vile facebook na twitter, ambayo hutumiwa na wengi enzi ya sasa. Jaji huyo ameahidi kuifanyia mageuzi makuu idara ya mahakama, kukiwamo kurejesha ofisi ya Msimamizi Mkuu wa Mahakama atakayekuwa na jukumu la kuhakikisha majaji na mahakimu wanakamilisha kesi zilizowasilishwa mbele yao kwa wakati. Wakati uo huo, ameahidi kuwapa haki ya kusikilizwa majaji ambao watakata rufaa baada ya kuachishwa kazi kupitia mchujo ulioendelezwa na kamati ya Sharad Rao.
Jaji Mbogholi amekuwa wa pili kuhojiwa baada ya jaji Alnashir Visram. Jumatano itakuwa zamu ya Jaji David Maraga.