Maafisa wa NOCK wachiliwa kwa Dhamana

Na, Sophia Chinyezi
Mahakama jumatatu imewaachilia kwa dhamana maafisa wawili wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki NOCK wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi na wizi wa mavazi ya wanariadha. Pius Ochieng ambaye ni Mwenyekiti na Katibu Mkuu, Francis Paul wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki mbili, huku wa tatu ambaye alikuwa kiongozi wa ujumbe wa Kenya jijini Rio, Brazil, Stephen Soi akikosa kufika mahakamani leo baada ya kuripotiwa kulazwa Nairobi Hospital. Soi ametakiwa kufika mahakamani Agosti 31 akiwa na stakabadhi za hospitali.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu Charity Oluoch amesema suala hilo litatajwa Septemba 19. Hata hivyo amewataka kufika katika Kitengo cha Kukabili Uhalifu wa Hali ya Juu na Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi mara mbili kila wiki kuanzia Ijumaa wiki hii.
Kadhalika ameagiza wasifike katika majengo yoyote yanayomilikiwa na NOCK, kutowasiliana na mashahidi kuhusu uchunguzi unaoendelea dhidi yao, kuwasilisha paspoti zao mahakamani mara moja na kutosafiri nje ya nchi bila idhini ya mahakama.
Awali upande wa mashtaka ulikuwa umeitaka mahakama kuwazuilia kwa siku ishirini na moja zidi ili wakamilishe uchunguzi wao.