Kwa kutongoza, wanawake mmedhihirisha hamna uwezo, nguvu, wala maneno matamu ya kuvutia

Dunia imepasuka, ujana unayumbayumba. Mengi yanababaisha huku machache yakisalia kuwa yalivyokuwa awali.

Aliyezoea kutafakari akianza kunena ujue kwamba kuna mengi ambayo hayaendi sawa. Sijui tunauasi Uafrika wetu au tumeiga wazungu kupita kiasi?

Kuhusu ninachokizungumzia najua kitakushangaza. Wiki haipiti bila kunena na mabinti wa aina ainati. Wengine marafiki huku wengine tunanena kimasomo. Naam! Masomo.

Ila kumetokea kundi lingine ambalo limekuwa likiniweka kwenye simu yangu muda mrefu zaidi na kukeshea simu karibu niitwe mwanga na watu wa kule kwetu Pwani. Lakini si kupenda kwangu, napenda kujuajua ndio maana marafiki hawa wapya nimekuwa nanena nao muda baada ya muda ili niskie na nijue walichonacho ambacho dunia yangu ndogo haina.

Usiku mmoja tukinena na mmoja wa marafiki hawa, alianza kunieleza jinsi usawa wa jinsia umeleta manufaa tele duniani katika karne ya sasa.

Binti huyu aliyependa mabadiliko katika majukumu ya jinsia aliniambia jinsi kule uzunguni, wanawake waliposea wanaume na hata kuwapa talaka.

Ahem! Hapo ndipo niligundua kuwa mada ilivyokuwa inanijia sipendi kuizungumzia haswa na watu wasionijua vyema.

Ubabe-dume wangu uliishia kunielekeza nimwarifu kuwa hakuna njia yoyote tungeuasi Uafrika wetu wa kudunisha wanaume kwa kuwa tumesoma au kuona wazungu wakifanya hivyo.

Kabla sijamalizia kauli zangu alianza kunichinjia kama asemavyo rafiki yangu fulani jijini. Sifa kuhusu kope, nyusi na hata urefu wangu zilimiminika.

Hapa nikajua fika kwamba nilikuwa nishanaswa. Sisemi kwamba kusifiwa ni kosa, ila ukisifiwa sehemu ambazo hujawahi wazia utakosaje kulegeza kamba na usikize zaidi? Ala! Kumbe hali huwa hii kwa wanawake!

Kabla hujanihukumu, kibaya zaidi ni kwamba alishindwa kusifia uzuri wa fikra zangu. Nikakasirika.

Nikagundua kwamba kumbe kutongoza ni kazi ya wanaume, wanawake hamna uwezo wa kutekeleza hili kwa umakinifu.

Ukitaka kumtongoza yeyote vyema hakikisha unaanza kusifia akili yake. Msitumie mistari iliyotumiwa na mababu zetu kuwapata nyanya. Wanawake mnapodhania kwamba mna uhuru wa kutenda mengi na karibu yote, acheni kutongoza wanaume.

Sekta hii mmedhihirisha hamna uwezo wala nguvu. Hamna maneno ya kuvutia ya kuambatana na tabasamu zenu. Twataka amani.

Ikiwezekana hakikisheni mnaenda shule au short-course mjue jinsi ya kuvizia, kutongoza na kumtia mfukoni bila kukalia wanaume chapati.

Ninapoandika makala ya leo, nipo pahali. Nimetulia. Namdekeza binti huyu aliyenijia kwa kujaribu kunivizia.

Namfunza jinsi ya kuvizia ili akafunze wengine. Usawa wa jinsia ni baraka kwetu tuliokuwa single. Wanatafakari hoiyeee!

Facebook: Stephen N Mburu

Twitter: MwandishiMburu