; /* Main responsive wrapper */ .player-wrapper { width: 100%; max-width: 900px; margin: 0 auto; padding: 10px; box-sizing: border-box; } /* Ensures controls are never clipped */ #atunwa-player { width: 100%; min-height: 320px; /* KEY FIX */ } /* Mobile landscape fix */ @media (orientation: landscape) and (max-height: 500px) { #atunwa-player { min-height: 260px; } }

UDA yatetea serikali kuhusu kashfa ya mafuta, yawashutumu wapinzani kwa siasa

Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar Sarai akiwahutibia wanahabari Mombasa Aprili, 06, 2026. [Robert Menza, Standard]
Chama tawala cha UDA kimetetea jinsi serikali inavyoshughulikia kashfa inayodaiwa kuhusiana na ununuzi wa mafuta, kikishutumu wapinzani wa kisiasa kwa kutumia suala hilo kwa manufaa binafsi na kuhatarisha usalama wa uchumi wa taifa.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Hassan Omar Sarai, chama hicho kimesema kuwa kundi la watumishi wa umma lilipanga njama ambayo ingeigharimu serikali zaidi ya shilingi bilioni tatu za Kenya.
Kulingana na UDA, maafisa hao walidaiwa kuvuruga mifumo ya usambazaji na kukwepa taratibu muhimu za upimaji wa ubora wa mafuta, wakijificha nyuma ya hofu ya uhaba wa mafuta nchini.
UDA imepongeza serikali pamoja na vyombo vya usalama kwa kuingilia kati na kusitisha kile ilichokiita jaribio la kuhujumu uchumi, huku ikiwahakikishia Wakenya kuwa bei ya mafuta itaendelea kuwa thabiti chini ya mfumo wa uagizaji wa mafuta kati ya serikali na serikali, unaojulikana kama 'G-to-G'.
Chama hicho pia kimeahidi kuwa hatua kali za kuhakikisha ubora wa mafuta zitazingatiwa, ikiwa ni pamoja na kufanya vipimo vya lazima kabla ya mafuta kuruhusiwa kuingia sokoni.
Wakati huo huo, UDA imemkosoa vikali aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na Ndindi Nyoro, ikiwatuhumu kwa kutoa matamshi ya “haraka na yasiyo na msingi", pamoja na kuwaunga mkono watu wanaodaiwa kuhusika katika njama hiyo.
Chama hicho kinasema viongozi hao hawakuwalaani wahusika na badala yake walichangia mkanganyiko miongoni mwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, njama hiyo ilihusisha kujaribu kuagiza mafuta kwa bei ya juu kwa kati ya shilingi 50 hadi 80 zaidi ya ile ya sasa chini ya mfumo wa G-to-G, hali ambayo ingeweza kusababisha mfumuko wa bei na kuyumbisha uchumi.
UDA imekanusha madai kuwa uagizaji mbadala ungepunguza gharama za mafuta, ikisema kuwa taarifa hizo zinapotosha umma.
Aidha, chama hicho kimesema kuwa taratibu za kurejesha fedha kutoka kwa waagizaji hao zimeanza, na kupendekeza adhabu ya hadi mara tano ya hasara iliyokadiriwa, sawa na takriban shilingi bilioni 15. Kiasi hicho, kinasema, kinaweza kuelekezwa katika kuimarisha hospitali za rufaa za ngazi ya sita.
UDA pia imevitaka vyombo vya uchunguzi kuchunguza matamshi ya Bw. Gachagua, ikidai huenda yanaashiria kuwa na taarifa ya awali kuhusu njama hiyo.
Chama hicho kimewataka viongozi wa kisiasa kote nchini kujizuia na kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko, kikionya kuwa kuingiza siasa katika masuala ya usalama wa uchumi kunaweza kuwa na athari kubwa kwa taifa.
Suala hili linajiri wakati dunia ikikabiliwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa mafuta, hali inayochangiwa na mivutano ya kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati, jambo ambalo UDA imesema linaongeza hatari kwa nchi kama Kenya kutumbukia katika misukosuko ya ugavi wa nishati.

.

RELATED NEWS