;

Bandari ya Lamu yapokea meli ya pili ya magari iliyogeuzwa njia kutokana na mzozo wa Iran

A cargo ship off loads containers at Lamu Port. [Omondi Onyango, Standard]
Meli ya Grande Florida Palermo, inayomilikiwa na kampuni ya Grimaldi Lines, imekuwa meli ya pili kubeba magari kugeuzwa kuelekea Bandari ya Lamu kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama unaohusishwa na mzozo unaoendelea nchini Iran.
Meli hiyo, iliyokuwa imebeba takriban magari 3,800 kutoka Yokohama, Japan, awali ilikuwa inaelekea Bandari ya Jebel Ali katika Dubai, Matiafa ya Milki za Kiarabu (UAE).
Hata hivyo, ililazimika kubadili mkondo kutokana na kuongezeka kwa hatari za kiusalama katika eneo la Ghuba, hali iliyosababisha kampuni ya usafirishaji kutafuta njia mbadala salama.
Meneja Mkuu wa Bandari ya Lamu, Kapteni Abdulaziz Mzee, amethibitisha kuwa hii ni mara ya pili kwa meli kama hiyo kugeuzwa ndani ya kipindi kifupi.
Meli ya kwanza iliwasili Lamu tarehe 11 Machi 2026 ikiwa imebeba magari 469 ambayo pia hayakuweza kufika katika soko lao la awali la Mashariki ya Kati.
Kapteni Mzee amesema magari kutoka kwa meli hizo yatahifadhiwa kwa muda katika bandari hiyo huku kampuni ya usafirishaji ikiendelea kutafuta njia salama na zinazowezekana za kuyasafirisha kwenda yalipokusudiwa.
Aidha, amebainisha kuwa mawakala kadhaa wa kampuni za usafirishaji wenye mizigo inayolenga Mashariki ya Kati wako katika mazungumzo na uongozi wa Bandari ya Lamu kuhusu uwezekano wa kupokea meli zaidi endapo hali ya usalama katika eneo la Ghuba itaendelea kuwa tete.
Mabadiliko hayo ya njia yanakuja wakati mzozo unaohusisha Iran, Marekani na washirika wake ukiendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa baharini katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mapigano yaliongezeka mwishoni mwa Februari 2026, yakihusisha mashambulizi ya kijeshi, ndege zisizo na rubani, na kuimarika kwa shughuli za kijeshi baharini katika eneo la Ghuba.
Mgogoro huo umeathiri hasa Mlango wa Hormuz, ambao ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji duniani, ambako sehemu kubwa ya biashara ya mafuta na mizigo hupita.
Kuongezeka kwa shughuli za kijeshi, mashambulizi dhidi ya meli na tahadhari za kiusalama kumelazimisha kampuni nyingi za usafirishaji kusitisha au kubadili safari zao ili kuepuka eneo hilo.
Ripoti zinaonesha kuwa meli kadhaa za kibiashara zimeharibiwa katika wiki za hivi karibuni, huku gharama za bima kwa meli zinazoingia eneo la Ghuba zikiongezeka kwa kasi, hali inayofanya baadhi ya njia kuwa hatari au ghali mno kuendesha.
Kutokana na hali hiyo, kampuni za usafirishaji zinageuza mizigo yao kuelekea bandari mbadala, ikiwemo za Afrika na Asia, huku zikisubiri hali ya usalama irejee kuwa ya kawaida.
Hali ya sintofahamu inayoendelea katika eneo la Ghuba inaweza kusababisha meli zaidi kuelekezwa katika bandari salama kama Bandari ya Lamu, jambo ambalo linaweza kuongeza shughuli za kibiashara katika kituo hicho kadri njia za biashara za kimataifa zinavyoendelea kubadilika.

.

RELATED NEWS