;

Kenya kuondoa maafisa wake wa polisi Haiti

Prime Cabinet Secretary Musalia Mudavadi during a one on one interview with The Standard group team on various issues in the country. [Wilberforce Okwiri, Standard]

Waziri mwenye Mamlaka Makuu, Musalia Mudavadi ametangaza kuwa maafisa wa polisi wa Kenya waliokuwa wametumwa nchini Haiti chini ya ujumbe wa kimataifa wa kurejesha usalama sasa wataanza kurejea nyumbani kufuatia kukamilika kwa jukumu la Multinational Security Support Mission (MSSM) na kuanzishwa kwa kikosi kipya kinachojulikana kama Gang Suppression Force (GSF).

Akizungumza katika taasisi ya Chatham House nchini Uingereza wakati wa hotuba yake iliyobeba mada “Kenya’s Expanding Foreign Policy Interests in a Changed World Order”, Mudavadi alisema ushiriki wa Kenya katika operesheni hiyo ulikuwa ishara ya dhamira ya nchi hiyo katika kulinda amani ya kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa mataifa katika kukabiliana na migogoro ya usalama duniani.

Mudavadi alisisitiza kuwa Kenya ilijiunga na operesheni hiyo kwa misingi ya mshikamano wa kibinadamu pamoja na uzoefu wake wa muda mrefu katika operesheni za kulinda amani.

“Ushiriki wetu uliongozwa na mshikamano wa kibinadamu pamoja na uzoefu wa Kenya katika operesheni za kusaidia kurejesha amani. Napenda kufahamisha kuwa Kenya imekamilisha jukumu lake kufuatia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2793 la mwaka 2025, lililobadilisha MSSM na kuanzisha kikosi kipya cha GSF,” alisema Mudavadi.

Aliongeza kuwa katika wiki zijazo kutakuwa na mchakato wa mwisho wa kuondoa kikosi cha Kenya huku maafisa waliokuwa nchini Haiti wakikamilisha mpito huo ili kuwezesha kikosi kipya cha Gang Suppression Force kuanza kazi rasmi katika juhudi za kurejesha usalama wa kudumu nchini humo.

Operesheni ya MSSM ilianza rasmi mwezi Juni mwaka 2024 baada ya Kenya na Haiti kusaini makubaliano ya ushirikiano yaliyoshuhudiwa na Rais William Ruto pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry mwezi Machi mwaka huo. Ujumbe huo uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) mwezi Oktoba 2023.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kenya kutuma kikosi cha kulinda amani katika eneo la Caribbean, hatua iliyochukuliwa wakati Haiti ilikumbwa na wimbi kubwa la ghasia za magenge ya wahalifu yaliyokuwa yakidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu Port-au-Prince.

Licha ya changamoto nyingi zilizojitokeza wakati wa operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kupoteza maafisa wawili wa polisi waliouawa wakiwa kazini, ujumbe huo uliripoti mafanikio kadhaa katika kuimarisha usalama na kusaidia taasisi dhaifu za serikali ya Haiti.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Christopher Landau alisema uwepo wa kikosi cha Kenya ulikuwa muhimu katika kuzuia kuanguka kwa serikali ya Haiti.

“Kwa uaminifu kabisa, serikali dhaifu ya Haiti isingeweza kustahimili mashambulizi ya magenge bila uwepo wenu,” alisema Landau wakati wa ziara yake nchini humo mwezi Januari alipokuwa akiwatunuku maafisa hao vyeti vya kutambua mchango wao.

Baada ya kikosi cha kwanza kutumwa nchini Haiti, Kenya ilipeleka vikosi vingine vitatu vya ziada vya polisi, ikiwa ni pamoja na maafisa 20 wanawake kutoka kikosi maalum cha SWAT cha Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

Maafisa hao walihudumu chini ya MSSM kabla ya kuhamia katika mpango mpya wa Gang Suppression Force, ambao sasa unatarajiwa kuendeleza juhudi za kukabiliana na magenge ya uhalifu na kurejesha uthabiti wa usalama nchini Haiti.

.

RELATED NEWS