;

Viongozi wakuu wa muungano wa upinzani wamshutumu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja

Viongozi wakuu wa Muungano wa Upinzani akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua [File]

Viongozi wakuu wa Muungano wa Upinzani wamemshutumu Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kwa kupuuza mkutano muhimu wa kiusalama katika Makao Makuu ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Jogoo House, wakisema hatua hiyo inaashiria kupuuzwa kwa masuala mazito ya usalama na kuongezeka kwa ukatili wa polisi pamoja na vitisho vya kisiasa.

Viongozi hao, akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa, waliwasili Jogoo House majira ya saa tano asubuhi, wakitarajia kukutana ana kwa ana na IG kufuatilia uchunguzi wa shambulizi la Kanisa la ACK Witima, lililotokea Othaya, Kaunti ya Nyeri mwezi uliopita.

Hata hivyo, dakika chache baada ya kuwasili, walitoka nje wakiwa wameghadhabika, wakidai kuwa IG hakuwepo licha ya kuwa ndiye aliyekuwa ameita mkutano huo. Walieleza kuwa aliondoka muda mfupi kabla ya wao kufika bila kuwajulisha, na badala yake kuwaachia maafisa wa ngazi za chini kuzungumza nao, jambo walilolikataa wakisema halikuzingatia uzito wa tukio hilo.

“Shambulizi dhidi ya mahali pa ibada ni kitendo cha kigaidi. Hili si suala la kawaida,” alisema Gachagua. “Ni Inspekta Jenerali pekee anayewajibika moja kwa moja kwa usalama wa nchi, na hatuwezi kujadili jambo hili na mtu mwingine.”

Kwa upande wake, Kalonzo Musyoka alisema walielekezwa kuzungumza na Msemaji wa Polisi, Muchiri Nyaga, lakini wakakataa wakisisitiza kuwa wanahitaji uwajibikaji wa moja kwa moja kutoka kwa mkuu wa jeshi la polisi. Aliongeza kuwa iwapo hawatapokea mwaliko mpya haraka, watarudi tena Jogoo House Ijumaa wiki hii.

Eugene Wamalwa naye alidai kuwa hali hiyo inaashiria kuingiliwa kwa majukumu ya polisi kutoka ngazi za juu za kisiasa, akisema upinzani hautalegeza msimamo hadi majibu ya wazi yatolewe. “Hili ni suala la uwajibikaji. Tutarejea hapa kila wiki hadi haki itendeke,” alisema.

Viongozi hao pia walihusisha malalamiko yao na vurugu zilizotokea katika mkutano wa kisiasa uliofanyika Kitengela na uliyoongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, ambapo kwa mujibu wa taarifa zao watu wawili walipoteza maisha na kadhaa kujeruhiwa kufuatia makabiliano kati ya waandamanaji na polisi.

Aidha, walilalamikia kuzuiwa kwao kuingia Nakuru kwa mkutano wa kisiasa, wakisema hatua hiyo ni jaribio la kukandamiza haki za kikatiba za kukusanyika na kujieleza.

“Polisi waliokabidhiwa jukumu la kulinda sheria na utulivu hawawezi kuwa chanzo cha hofu kwa wananchi,” alisema Gachagua. “Silaha zilizonunuliwa kwa fedha za walipa kodi kulinda maisha ya Wakenya haziwezi kuelekezwa kwa raia wasio na hatia.”

Upinzani sasa umeapa kuendelea kushinikiza uwajibikaji wa juu kabisa katika uongozi wa polisi, ukisema hautanyamaza hadi majibu ya kuridhisha yatolewe na hatua stahiki kuchukuliwa.

.

RELATED NEWS