×
App Icon
The Standard e-Paper
Home To Bold Columnists
★★★★ - on Play Store
Read on the App

Kesi ya Shakahola kuchukua mkondo mpya: Mlinzi wa mackenzie aomba kukiri

...

Huenda kesi ya mauaji ya Shakahola inayomkabili mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie pamoja na washukiwa wengine ikachukua mkondo mpya, baada ya mmoja wa washukiwa kuonyesha nia ya kukiri na kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyotendeka katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Mahakama Kuu imeagiza mshukiwa katika mojawapo ya kesi za mauaji ya Shakahola kuandika na kurekodi ungamo jipya, ili kutoa maelezo kamili kuhusu uhalifu unaodaiwa kutekelezwa katika msitu huo kati ya mwaka elfu mbili na ishirini na elfu mbili na ishirini na tatu, kipindi ambacho watu 429 walipoteza maisha.

Mshukiwa huyo ni Enos Amanya, anayefahamika pia kwa jina Haleluya, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha usalama cha Paul Mackenzie ndani ya msitu wa Shakahola.

Jaji wa Mahakama Kuu, Diana Mochache, amekubali ombi la mshukiwa huyo la kurekodi ungamo jipya, na kuagiza kwamba asindikizwe hadi ofisi ya DCI Kanda ya Pwani chini ya usimamizi wa afisa anayechunguza kesi hiyo.


Jaji Mochache amesisitiza kuwa Haleluya lazima afafanue kwa kina makosa aliyoyatenda, pamoja na kueleza iwapo kulikuwa na ushiriki wa washukiwa wenzake katika matukio ya mauaji hayo.

Wakati wa kurekodi ungamo hilo, mahakama imeamuru kwamba Haleluya aambatane na binti yake au shahidi mwingine atakayemchagua, kama sehemu ya kuhakikisha uwazi wa mchakato huo.

Ombi hilo liliwasilishwa na wakili wake, Kelvin Lisanza, aliyefahamisha mahakama kuwa ungamo la awali lililorekodiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu David Odhiambo halikujumuisha vipengele muhimu vya kesi hiyo.

Kwa mujibu wa Lisanza, baadhi ya taarifa ziliachwa nje wakati wa kurekodi ungamo hilo, na kuomba muda zaidi kwa mteja wake kutoa maelezo ya kina.

Mahakama pia ilielezwa kuwa ungamo la awali lilirekodiwa kati ya saa kumi na moja jioni hadi saa moja usiku, wakati ambao mshukiwa alikuwa amechoka baada ya kuhudhuria vikao vya kesi mbalimbali.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa taarifa iliyorekodiwa awali ilikuwa na maswali ya jumla ambayo hayakugusa moja kwa moja masuala muhimu ya mauaji ya Shakahola au nafasi ya kila mshukiwa katika uhalifu huo.

Mawakili wa mashtaka, wakiongozwa na Naibu Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma Joseph Kimanthi, wamesema kuwa nyaraka za awali za kurasa thelathini na tatu hazikukidhi vigezo vya kisheria vya kuhesabika kama ungamo halali.

Wameongeza kuwa baadhi ya kurasa za ungamo hilo zilikuwa zimepotea na kwamba mshukiwa hakujitwika lawama wala kuwataja washukiwa wenzake.

Upande wa mashtaka pia umependekeza kwamba Afisa Mkuu wa Polisi mwenye cheo cha Chief Inspector aandike ungamo jipya kwa kutumia maswali mahsusi, na hata kupendekeza mshukiwa huyo kukiri hatia upya ili kuruhusu ukweli wa kesi kusomwa na kufungua njia ya hukumu kutolewa.

Enos Amanya, ambaye alikuwa miongoni mwa kikosi cha usalama cha Mackenzie msituni Shakahola, anasemekana kujitolea kwa hiari kukiri makosa yake, akisema anafanya hivyo kwa ajili ya kutafuta haki kwa waathiriwa na familia zao.

Kwa sasa, Haleluya anakabiliwa na mashitaka 191 ya mauaji pamoja na Paul Nthenge Mackenzie na washukiwa wengine 29.