×
App Icon
The Standard e-Paper
Informed Minds Prefer The Standard
★★★★ - on Play Store
Download Now

Mswada wa tawahudi (autism) walenga kuwasaidia waathiriwa na familia zao

Waziri wa Leba na Maswala ya Wafanya kazi Florence Bore wakati wa uzinduzi wa ripoti ya tawahudi Januari 31, 2024. [Edward Kiplimo, Standard]

Mswada mpya unaolenga kuanzisha mwongozo wa kitaifa kwa ajili ya utambuzi wa mapema, uchunguzi na usimamizi wa tawahudi (autism), huku ukihamasisha uelewa na kutenga rasilimali za kuwasaidia waathiriwa pamoja na familia zao.

Mswada wa Usimamizi wa tawahudi (Autism) wa mwaka 2025, ambao kwa sasa unachunguzwa na Kamati ya Seneti inayohusiana na masuala ya Afya, unapendekeza kuanzishwa kwa vituo maalumu vya uchunguzi, kuwapa mafunzo wataalamu wa afya na walimu, na kuhakikisha huduma za usimamizi wa tawahudi zinatolewa kwa uratibu katika ngazi ya kitaifa na kaunti.

Mswada huo, uliodhaminiwa na Seneta Karen Nyamu, unapendekeza mfumo mpana wa kushughulikia mapungufu yaliyopo katika uchunguzi wa mapema, utoaji wa huduma maalum, mafunzo, pamoja na ukusanyaji wa data.


Unaitaka Serikali ya Kitaifa kutengeneza viwango vya kitaifa na Mkakati wa Kitaifa wa tawahudi (Autism), kuanzisha vituo vya uchunguzi katika hospitali za rufaa, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na walezi, kuhamasisha umma, na kuunda hazina ya kitaifa ya data kwa madhumuni ya kupanga na kutoa huduma.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), matatizo ya wigo wa tawahudi (ASD) ni kundi tofauti la hali zinazoonekana kwa changamoto katika mwingiliano wa kijamii na mawasiliano. Dalili nyingine ni pamoja na mifumo ya tabia na shughuli zisizo za kawaida ikiwa ni pamoja na ugumu wa kubadilika kutoka shughuli moja hadi nyingine, kuzingatia kwa kupita kiasi mambo madogo na miitikio isiyo ya kawaida kwa hisia.

Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa watoto wanaogunduliwa kuwa na tawahudi, pamoja na wazazi wao, wana uwezekano mkubwa wa kuwa wameathiriwa na baadhi ya sababu za kimazingira.

Wanasayansi hata hivyo wamebaini hali kadhaa zinazoonekana kuwa za kawaida kwa waathiriwa kama vile umri mkubwa wa wazazi, na ugonjwa wa kisukari kwa mama wakati wa ujauzito. Kuzaliwa kabla ya wakati, matatizo makubwa wakati wa kujifungua na uzito mdogo wa mwili pia yamehusishwa na ongezeko la uwezekano wa kupata tawahudi.

Mswada wa Nyamu unaelekeza kuwa serikali za kaunti zitapaswa kuanzisha vituo vya uchunguzi katika hospitali za ngazi ya 4 na 5, kuweka makundi ya usaidizi kwa walezi katika jamii, kuunda hifadhidata za kaunti kuhusu tawahudi na kutenga fedha kwa huduma za kuzuia na usimamizi. Aidha, ngazi zote mbili za serikali zitaanzisha vitengo vya tawahudi kwa ajili ya kuratibu programu, kukusanya data na kuendesha kampeni za uelimishaji kwa umma.

“Mswada huu unalenga kuweka mbinu jumuishi na iliyoratibiwa ya usimamizi wa tawahudi (autism) nchini Kenya. Aidha, unalenga kuanzisha mfumo kamili wa kisheria kwa uchunguzi wa mapema, utambuzi, usimamizi na uhamasishaji wa umma, pamoja na kuhakikisha kutengwa kwa rasilimali za kutosha kwa programu za autism,” sehemu ya mswada huo inasema.

Mswada huo pia unaitaka Taasisi ya Kuandaa Mitaala ya Kenya (KICD) kujumuisha elimu kuhusu tawahudi katika mafunzo ya walimu kabla ya kuingia kazini na wakati wakiwa kazini, na kuandaa mitaala kuhusu usimamizi wa autism katika ngazi zote za elimu.

Nyamu alisema sheria hiyo inalenga kukabiliana na changamoto kama vile kuchelewa kugundua tatizo, uhaba wa wataalamu waliobobea, ukosefu wa huduma maalumu, na kutokuwepo kwa data sahihi ya kitaifa kuhusu idadi ya waathiriwa wa tawahudi.

Aidha, alibainisha kuwa mswada huo unaendana na azimio la kimataifa la WHO la mwaka 2014 kuhusu tawahudi, na pia unaimarisha Kifungu cha 43(1)(a) cha Katiba kinachohakikisha haki ya kupata viwango bora zaidi vya afya.

Ili wananchi washiriki katika mchakato huo, Seneti imealika watu wote kutoa maoni yao kuhusu sheria hiyo inayopendekezwa. Mswada huo, uliosomwa kwa Mara ya Kwanza tarehe 26 Novemba 2025, sasa upo wazi kwa ushiriki wa umma kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 118 cha Katiba na Kanuni ya Kudumu 145(5).

Maoni yote lazima yafikishwe kabla ya saa 11:00 jioni, Jumatatu, Desemba 22, 2025.