×
App Icon
The Standard e-Paper
Home To Bold Columnists
★★★★ - on Play Store
Download Now

Boni Khalwale angatuliwa kama kinara wa walio wengi bunge la Seneti

 

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale akiwahutubia wanahabari nje ya majengo ya bunge. [Elvis Ogina, Standard]

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, ameondolewa rasmi katika nafasi ya Kiranja wa Wengi katika bunge la Seneti baada ya muungano wa Kenya Kwanza wenye wabunge wengi kupitisha azimio la kumwondoa.

Hatua hiyo imefungua ukurasa mpya katika uongozi wa Seneti, huku Seneta wa Bungoma, David Wafula Wakoli, akichaguliwa kuchukua nafasi hiyo mara moja.


Tangazo la mabadiliko hayo liliwasilishwa rasmi kwa Seneti na Spika Amason Kingi siku ya Jumanne.

Kingi alithibitisha kuwa uamuzi huo ulizingatia taratibu zote za kisheria na masharti ya Kanuni za Kudumu, hasa Kanuni ya 22 inayohusu uteuzi na mabadiliko ya viongozi wa wengi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Spika, mabadiliko hayo yalitokana na mkutano wa wabunge wa muungano wa wengi uliofanyika Desemba 2.

Kumbukumbu za kikao hicho, pamoja na orodha ya waliouhudhuria, ziliwasilishwa kwa ofisi yake na Kiongozi wa Wengi, Aaron Cheruiyot.

Nyaraka hizo zilionyesha kuwa maseneta waliamua kumuondoa Khalwale kwa mujibu wa Kanuni ya Kudumu 22(5) na kumchagua Wakoli kuchukua nafasi hiyo.

“Nimeridhika kuwa mabadiliko haya yameafikiwa ipasavyo na yanakidhi vigezo vinavyotakiwa. Kwa hivyo mhudumu rasmi wa ofisi hii sasa ni Seneta David Wafula Wakoli,” alisema Spika Kingi.

Kuondolewa kwa Khalwale kunachukuliwa kama mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi wa Kenya Kwanza ndani ya Seneti, yakibainisha pengo la kisiasa lililokuwa likichipuka katika miezi ya hivi karibuni.

Akiwa Kiranja wa Wengi, Wakoli atasimamia ajenda ya serikali ndani ya Seneti, kuhakikisha nidhamu ya wabunge wa muungano na kuratibu upitishaji wa miswada na hoja muhimu za serikali.

Khalwale, akizungumzia hatua hiyo, alitoa kauli fupi na ya mafumbo: "A day in politics..."  akionekana kukubaliana kimyakimya na hali halisi ya kisiasa.

Hapo awali, Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, alikuwa mmoja wa wanaotaka Khalwale aondolewe. Alimshutumu kwa kuunga mkono mgombea aliyekuwa nje ya chama cha UDA katika uchaguzi mdogo wa Malava.

Wakati wa kampeni, Khalwale alionekana akifanya kazi na viongozi wa upinzani, akiwemo Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, na kiongozi wa DAP–Kenya, Eugene Wamalwa, wakimpigiia debe Seth Panyako.

Katika matokeo ya uchaguzi huo, Panyako alipoteza, huku mgombea wa UDA, David Ndakwa, akishinda katika kinyang’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali.