Lewis Kazungu, mshukiwa mkuu wa mauaji ya Farida Kadzo, msichana wa miaka 17 ameomba mahakama iruhusu mazungumzo ya makubaliano ya kipekee na upande wa mashtaka.
Kazungu anadaiwa kumuua Kadzo kwa kumdunga kisu Juni 6, eneo la Mferejini, Kijipwa Kaunti ya Kilifi baada ya mzozo wa kimapenzi.
Kupitia mawakili wake, Kazungu ameomba fursa ya kuingia katika mpango wa makubaliano ya kujadiliana kwa makosa ya jinai, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kupata suluhu ya haraka na yenye manufaa kwa pande zote.
Mawakili wake wamesisitiza kuwa makubaliano hayo huenda yakachangia kwa kiasi kikubwa katika kuepusha usikilizaji wa kesi ndefu, ambayo mara nyingi hutumia rasilimali nyingi za mahakama na kuwaumiza zaidi wahusika na familia.
Aidha, wamesema Kazungu yuko tayari kushirikiana kikamilifu na kutii masharti yoyote yatakayoambatana na mpango huo, ikiwa utapitishwa na upande wa mashtaka. Wamesema lengo lao ni kuhakikisha haki inatendeka huku pia wakichangia katika juhudi za ukarabati na ufumbuzi wa haraka wa kesi hiyo ambayo imekuwa ikivutia hisia kali za umma.
Kwa upande wake, mashtaka yameiomba Mahakama Kuu ya Mombasa muda wa siku 14 ili kupitia ombi hilo na kufanya mashauriano ya kina kabla ya kutoa msimamo rasmi.
Wakili wa serikali ameiambia mahakama kuwa suala hilo ni zito na linahitaji muda wa kutosha kufanyiwa tathmini, ikiwemo mashauriano na familia ya marehemu pamoja na wadau wa haki ya jinai.
Jaji Wendy Kagendo amekubali ombi la upande wa mashtaka na kuagiza kesi hiyo kurejea kwa usikilizaji mnamo tarehe 18 Desemba, wakati ambapo mahakama inatarajiwa kusikia iwapo pande zote zimeafikiana kuhusu kuingia katika makubaliano.
Wakati huo huo, shirika la International Justice Mission (IJM) linaendelea kufuatilia kwa karibu kisa hiki, likisema lengo lake ni kuhakikisha kuwa familia ya Farida Kadzo, aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Upili ya Ng’ombeni, inapata haki kamili.
Farida, aliyekuwa mtoto wa pili katika familia ya watoto sita, pia alikuwa mama wa mtoto mchanga wa miezi tisa, hali iliyozua masikitiko makubwa katika jamii ya Kijipwa na maeneo ya Jilore na Kibarani ambako familia yake ina uhusiano.
Kesi hii imeendelea kuibua mjadala kuhusu usalama wa wasichana, unyanyasaji wa kijinsia, na hatua zinazochukuliwa na serikali kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika Kaunti ya Kilifi na maeneo ya Pwani kwa ujumla.