Papa Francis, kukutana na waathiriwa wa machafuko nchini Sudan

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis leo Jumamosi atakutana na waathiriwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na viongozi wa kidini nchini Sudan Kusini katika siku ya pili ya ziara yake kwenye taifa hilo linalokabiliwa na machafuko.

Mkutano huo unafuatia wito alioutoa Papa Francis siku ya Ijumaa kwa viongozi wa Sudan Kusini akiwataka kutafuta amani ya kudumu na kukomesha mateso yanayowakumba raia.

Papa Francis aliyewasili nchini Sudan Kusini Ijumaa Alasiri baada ya ziara yake katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, tayari amefanya mazungumzo na rais Salva Kiir.

Amewashauri viongozi wa taifa hilo changa kumaliza machafuko nchini humo yanayosababisha madhila ya kila siku kwa raia.

Rais Kiir alikuwa pamoja na hasimu wake wa muda mrefu ambaye pia ni makamu wa rais Riek Machar wakati alipomkaribisha Papa Francis kwenye bustani ya Ikulu ya Rais mjini Juba.