×

Rais Ruto atoa ahadi ya kuimarisha Ushirikiano wa Kenya na Tanzania

Rais William Ruto na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, wameahidi kushirikiana kuimarisha urafiki kati ya Kenya na Tanzania, kukiwamo kuondoa vikwazo vya kibiashara kwenye mipaka ya mataifa haya mawili.

Aidha, Rais Ruto amekariri kwamba ataendeleza ushirikiano uliowekwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta kwa manufaa ya raia wa nchi hizi mbili.

Rais Ruto amesema jambo la kwanza mara tu mawaziri wake watapoapishwa, litakuwa kutafuta jinsi vikwazo vyote 14 vilivyosalia vya kibiashara kati ya Kenya na Tanzania vinavyoweza kuondolewa.

Baadhi ya vikwazo ambavyo Ruto ameahidi kushughulikia ni kama vile ucheleweshaji wa kibali cha bidhaa kutokana na uchunguzi wa muda mrefu wa forodha nchini Kenya; ucheleweshaji wa leseni ya kuagiza bidhaa za maziwa kwa Watanzania; masharti ya KRA dhidi ya matumizi ya bidhaa za Tanzania, vikwazo kwa wataalamu wa Kitanzania kupata kazi nchini Kenya; Cheti cha chanjo ya Covid-19 ya Kenya kwa wasafiri wa anga kutoka Tanzania; na ugumu wa Kampuni ya Taifa Gas ya Tanzania kuwekeza nchini Kenya.

Aidha, Kenya pia inatarajia Tanzaia kuondoa vikwazo vya kukataa tenda za wahandisi wa Kikenya, kukataliwa kwa zabuni ya Jambojet ya Kenya kuendesha huduma za ndege nchini Tanzania; na vikwazo dhidi ya magari ya watalii kutoka Kenya katika mpaka wa Namanga.

Vilevile, kuna mgogoro wa utozaji ushuru kwenye mipaka ya Kenya na Tanzania, ambao umeathiri undugu wa nchi hizi mbili.

Tofauti na awali, Rais Ruto amesema tayari baadhi ya vikwazo vimeondolewa kwa manufaa ya raia wa mataifa haya mawili.

Katika kikao cha pamoja na mwenyeji wake Samia Suluhu, Ruto ambaye yuko Tanzania kwa ziara ya siku mbili, amepongeza juhudi zilizowekwa na watangulizi wa mataifa haya mawili wakiwamo aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Julius Nyerere na Hayati Jomo Kenyatta.

Wawili hao wameahidi kuendeleza urafiki wa nchi hizi mbili, Ruto akiahidi kukamilisha mradi wa bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Mombasa, mradi ulioanzishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Samia Suluhu amesema awali vilikuwapo vikwazo takribani 68 vilivyotishia undugu wa Kenya na Tanzania, na kwamba majadiliano yalifanywa kati yake na Mstaafu Kenyatta ambapo vikwazo hamsini na vinne viliondolewa.

Rais Ruto amesema mataifa haya mawili yatajitahidi kuongeza biashara maradufu kutoka shilingi bilioni 90 za sasa ili kuwanufaisha raia wa pande zote mbili.

Takwimu za Benki Kuu ya Kenya, CBK zinaonesha kwamba mwaka wa 2021, mauzo ya bidhaa za Kenya kwenda Tanzania yalipanda juu zaidi kwa asilimia 46 hadi shilingili bilioni 28.66, ambapo Tanzania ilinufaika pia baada ya mauzo yake kupanda kwa asilimia 43.39 hadi shilingi bilioni 45.6.