Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma wameghadhabishwa na hatua ya Wizara ya Elimu, Hazina Kuu na Baraza la Ushauri la Vyuo Vikuu vya Umma IPUCCF, kukosa kutimiza ahadi waliyotoa walipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Elimu wiki iliyopita kwamba watawasilisha mkataba bora kwa vyama vyao ili kusitisha mgomo unaoendelea.
Wakizungumza na wanahabari, viongozi wa vyama vya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu UASU na KUSU, wamesema badala yake siku ya Jumamosi, IPUCCF iliwasilisha stakabadhi waliyodai kwamba ulikuwa mkataba mwingine, stakabadhi ambayo wameitaja kuwa bandia na ambayo haikuafikia viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria. Mwenyekiti wa UASU, Muga K'Olale amesikitishwa na hatua ya Waziri wa Elimu na Makatibu wa Elimu ya Juu na wa Hazina Kuu kwa kutoweka mikakati ya kushughulikia malalamiko waliyoibua.