Since 1902

Kiunjuri ang’atwa na nzige wa Uhuru

Aliyekuwa waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri.

Mabadiliko ya baraza la mawaziri ya Rais Uhuru Kenyatta yanaendelea kupokelewa kwa mikono tofauti na hisia mbali mbali haswa baada ya kumtimua kazi waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri.

Nafasi yake imechukuliwa na Peter Munya. Kiunjuri amefungashwa kuelekea nyumbani wakati wizara yake inazuzushwa na Nzige ambao wanaendelea kuvamia maelfu ya mimea na mazao kaskazini mwa Kenya.

Miongoni mwa ngonjera yake katika kupambana na uvamizi wa nzige, Kiunjuri anakumbukwa kuwaambia Wakenya kwamba wakiona mdudu yeyote karibu nao, wamchukue picha yake ili kuiwezesha serikali (wizara) kufahamu kana kwamba ni nzige.

Sasa wadadisi wa siasa wanazungumzia pia matamshi yake ya hivi majuzi dhidi ya mchipuko wa jopo kazi la BBI kuwa miongoni sababu nyingine za kula wembe.

Siasa za 2022 hali kadhalika zimemtongea kutokana kwamba daima amekuwa akiimba wimbo wa kura za urais za 2022 kinyume cha agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

Ikiwa ni nzige na BBI ndiyo ambayo imemla Mwangi Kiunjuri, je, kunao uwezekano mwingine kwamba mtandao wa Naibu Rais William Ruto unazidi kumenywa kama njia mojawapo ya kumlegeza kisiasa ya 2022?

Kubanduliwa kwa Kiunjuri kunazidisha kutonesha kidonda cha kisiasa cha mrengo wa naibu Rais na kutoa ishara kwamba huu ndio mwanzo wa ngoma kabla ya midundo zaidi ya BBI kujibwagiza kufi kia katikati mwa mwaka huu.

Je, BBi ni daraja la utengano? “Ikiwa kila Mkenya amekubiliana na mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya BBI, kuna sababu gani ya kufanya mikutano ya kuwarai Wakenya kuiunga mkono ilihali ni wazi kwamba kila mtu anakubaliana na mapendekezo ya ripotii hiyo?’’

Ni matamshi yake Naibu wa Rais Daktari William Ruto.

Baada ya matamshi haya yenye kupenya hadi mioyoni mwa Wakenya, mjadala umezuka katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba uhusiano kati ya Rais uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt.William Ruto unaendelea kudorora ikilinganishwa na miaka ya awali ambapo Rais Na Naibu wake wangevalia suti za Rangi sawa sawia na sare za wanafunzi, hiyo ikiwa ni njia ya kupitisha ujumbe kwa wapinzani wao wa kisiasa jinsi walivyoaminiana.

Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanahoji kwamba muungano wa ‘UhuruRuto’ ulibuniwa kwa ajili ya kupambana na jinamizi la kesi za ICC na ungesambaratika punde baada ya kesi zao kutupiliwa mbali.

Aidha mtego wa kumnasa Naibu wa Rais uliowekwa na wana kieleweke wanaounga mkono ushirikianp wa Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga unaonekana kuwanasa wao wenyewe kwani Naibu wa Rais alikubali ripoti ya BBI kinyume na matarajio yao, jambo ambalo limerudisha kikosi cha ‘Timu BBI’ mezani kuchora upya ramani ya siasa za baadae nchini.

Hatua ya Naibu wa Rais kukwepa viunzi vya wapinzani wake pia imechukuliwa kuwa mwanzo wa makabiliano ya kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kwa upande mmoja na Raila Odinga upande wa pili.

Mvutano huu ni wa aina yake kwani Ruto anasajili jina lake kwenye daftari za kumbukumbu kama Naibu wa pekee wa Rais kwenye historia ya Kenya huru kwenda kinyume na mipangilio ya serikali na hasa msimamo wa Rais ambaye ametwikwa mamlaka ya kutoa mwongozo serikalini kikatiba.

Kero kwa Ruto Wananchi wengi wanaoshiriki mijadala hii mitandaoni na vyombo vya habari wanaonekana kufurahishwa na matamshi ya Naibu wa Rais anayeonekana kukerwa na hatua ya wizara ya usalama wa ndani na uratibu wa serikali ya kitaifa chini ya uongozi wake Waziri Dr. Fred Matian’gi kuandaa mikutano maeneo ya kaunti ili kukipigia debe ripoti ya BBi ambayo tayari inaungwa mkono kwa kiwango kukubwa na Wakenya.

Ruto anasisitiza kwamba huo ni mpenyo wa ubathirifu wa fedha za umma. Mikutano hiyo aidha imeonekana kutumika kama jukwaa la kubuni miungano ya kisiasa kwa ajili ya kinyan’ganyiro cha Ikulu mwaka 2022.

Kauli ya Mbunge Mteule wa chama cha Jubilee, Maina Kamanda kwenye mkutano wa kundi la BBI mjini Kisii ya kuwaomba wakaazi wa eneo la Nyanza kumuunga mkono waziri Matian’gi na kumtaka Raila na Uhuru kumjumuisha katika serikali ijayo kama waziri mkuu yamezua tumbo joto miongoni mwa wafuasi wa kundi la ‘Tanga Tanga’ ambao wanaamini kwamba BBI hhaijatumika kama chombo cha kisiasa bali ni njia ya kuwaunganisha wakenya.

Matamshi ya Maina Kamanda yamezua mfarakano zaidi na kuwaacha wandani wa kisiasa wa Naibu Rais wakitafakari na kutathmini upya uamuzi wao wa awali wa kuunga mkono ripoti ya BBI kwa sharti la kuwa ropiti hiyo ittoa nafasi ya kuboresha maisha ya Wakenya.

Kundi hilo pia linahofi a kuhujumiwa kwa mipango ya chama cha Jubilee ya kutumia mijadala juu ya ripoti hiyo kuzua hoja mpya ya kinyanganyiro cha urais mwaka 2022.

Wandani wa Naibu wa Rais wanadai kwamba Raila Odinga tayari amebuni muungano mpya wa kisiasa kwa ajili ya kuusajili kuwa chama kuingia kwenye uchaguzi wa mwaka 2022 na anazunguka kote nchini kukitaftia chama hicho uungwaji mkono.

Mbunge wa Kiminini Didimus Barasa anadai kwamba Raila amemtenga kigogo wa Ukambani Stephen Kalonzo Musyoka na kuwaleta kar ibu Magavana Alfred Mutua na Charity Ngilu na hivi punde zaidi amemuondoa Msalia Mudavadi na badala yake kumleta waziri Eugene Wamalwa.

Hata hivyo kundi la viongozi wanaounga mkono Ripoti hiyo maarufu kama ‘Team BBI’ linayowajumuisha wana ‘Kieleweke’ na kundi la wabunge kinadada la ‘Embrace’ linawalaumu wenzao wa Tanga Tanga na kundi la ‘Inua Mama’ kwa kuanzisha kampeni za mapema za uchaguzi wa mwaka 2022 hata kabla ya kutolewa kwa mapendekezo ya jopo kazi la BBI.

Mkuki kwa nguruwe Mbunge mteule wa ODM Geofry Osotsi naye amemsuta Naibu wa Rais kwamba analalamika bila sababu huku akimnyoshea kidole kuwa Ruto ndiye aliyeyaanzisha kampeni za mapema za uchaguzi wa mwaka 2022.

Seneta wa kakakamega Cleopas Malala vilevile anamsuta Naibu wa Rais kwa kuhofi a asilolifahamu, ‘BBI ni mradi wa Rais yeye anapaswa kujadili swala lolote asilokubaliana nalo na mkuu wake, amesema Malala.

Hofu kuu ya wakenya ni kupoteza nafasi ya kutoa mchango wao kwani nafasi iliyotolewa ili Wakenya waweze kuisoma na kutoa maoni kwenye awamu ya pili imetekwanyara na wanasiasa wanaotumia nafasi hiyo kama uga wa mashindano ya uchaguzi wa mwaka 2022 na kubuni miungano.

Swala la pili linalokatisha tamaa mwananchi ni kutokuwepo kwa nakala za kutosha miezi miwili baada kutolewa kwa ripoti hiyo.