Ukumbusho wa Kijana Wamalwa wafanyika

Na, Martin Ndiema
Ukumbusho wa Kijana Wamalwa wafanyika
Maadhimisho ya 14 tangu kufariki dunia kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Kijana Wamalwa yamefanyila leo hii nyumbani kwake mjini Kitale Kaunti ya Trans Nzoia huku suala kuhusu uchaguzi mkuu uliokamilika likishamiri. Aidha viongozi wengine waliohutubu halfa hiyo wameyakosoa matamshi yanayotolewa kuhusu uwezekano wa kuligawanya taifa kwa misingi ya miegemeo ya kisiasa.
Akihutubu wakati wa hafla hiyo, kakaye marehemu ambaye ni Waziri wa Maji, Eugene Wamalwa amewapongeza wakazi wa eneo la Magharibi ya Nchi kwa kuwahakikishia ushindi baadhi ya wanasiasa waliowania viti vya uongozi kupitia Chama cha Jubilee.
Aidha kauli ya Mwanauchumi na Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa, David Ndii ya kuunga mkono kugawanywa kwa taifa hili kwa misingi ya kisiasa, imeibua hisia miongoni mwa viongozi waliohudhuria ibada hiyo. Mbunge mteule wa Kimilili, Ditmus Barasa na mwenzake wa Endebess, Daktari Robert Pukose wamewarai maafisa wa usalama kumchukulia Ndii hatua kali za kisheria.  Kauli ya viongozi hao imetiliwa mkazo na Mbunge mteule wa Sirisia John Waluke.  
Si hayo tu, aliyekuwa Mbunge wa Matungu David Were na mwenzake wa Saboti, David Lazarus wamewashauri Wakenya kudumisha amani.
Kijana Wamalwa alikuwa Makamu wa Rais wakati wa utawaka wa Rais Mstaafu, Mwai Kibaki na alifariki dunia mwaka 2003 baada ya kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miezi minane.

Related Topics