11th February, 2019
Wakulima nchini watalazimika kusubiri zaidi kupokea mbolea ya bei nafuu kutoka kwa serikali, huku wizara ya kilimo kupitia halmashauri ya nafaka nchini ncpb ikiwa bado haijawajibikia matumizi ya takriban shilingi bilioni 2.1. Waziri wa kilimo mwangi kiunjuri ameeleza kamati ya bunge kuwa japo uchunguzi bado haujakamilika, wizara hiyo inaweza aidha kuagiza mbolea kupitia mfumo wa ununuzi ulioidhinishwa chini ya kipengee 114 cha sheria kuhusu ununuzi wa bidhaa, au kupitia makampuni ya binafsi. Hata hivyo, amefafanua kuwa endapo utaratibu utakaokubalika ni ununuzi kwa mujibu wa kipengee 114, wakulima bado watasubiri siku 21 kabla ya kupokea mbolea. Kwa mujibu wa kamati ya bunge, taifa linakodolea macho hatari ya uhaba wa chakula endapo suluhu ya haraka haitapatikana, kwa kuwa msimu wa upanzi unatarajiwa kuanza kufikia mwishoni mwa mwezi huu.