Rais William Ruto ameweka wazi kwamba yuko tayari kwa mazungumzo na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.
Hata hivyo, Rais Ruto ambaye amezungumza katika Kaunti ya Bomet wakati wa uzinduzi wa barabara ya kilomita 75, amesema kuwa hawezi kukubali vitisho vya Azimio kukiwamo kurejelea maandamano ya kila wiki Jumanne ijayo.
Ruto aidha ameapa kutumia asasi zote za serikali kuwalinda Wakenya na mali zao wakati wa maandamano. Kauli yake imesisitizwa na Naibu wake Rigathi Gachagua.
Viongozi wengine walioandamana na Ruto akiwamo Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wah wameapa kuendelea kushirikiana na rais katika kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.
Viongozi hao wamemtaka Ruto kutotishwa na mashinikizo ya Azimio.
Rais awali aliongoza ufunguzi wa Kampuni ya Nafaka ya Grain Bulk Handlers Limited tawi la Nairobi akiandamana na wandani wake ambapo aliahidi kupunguzwa hadi shilingi mia moja kwa bei ya unga wa mahindi kuanzia wiki ijayo.