×
× Digital News Videos Opinion Special Reports Lifestyle Weird News Health & Science Education Columns The Hague Trial Kenya @ 50 Comand Your Morning E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian Entertainment Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
×

Sasa uchimbaji mchanga baharini waumiza uvuvi

By Mohamed Seif | November 27th 2019 at 09:45:47 GMT +0300

Uchimbaji mchanga baharini unaoendelea sasa ni tishio kubwa kwa wavuvi wa kaunti za Mombasa na Kwale.

Utafiti umeonyesha kwamba uvuvi na biashara ya samaki kaunti za Kwale na Mombasa zimepata pigo kubwa kutokana na uchimbaji mchanga wa baharini.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti ilozinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia uchunguzi wa athari za shughuli za uchimbaji wa mchanga wa baharini.

Wadau kwenye nyanja husika wamekuwa wakilipigia kelele suala la uchimbaji wa mchanga uliotekelezwa ili kutumikia ujenzi wa miradi mikubwa ya miundo msingi.

Hususan wadau kwenye sekta za utalii, uvuvi na hata wakereketwa wa mazingira ya baharini walikerwa sana na shughuli hizo kuanzia mnamo 2016.

 Wakati huo uchimbaji wa mchanga ulifanywa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa SGR. Mapema mwaka huu suala hilo likachipuka tena, mara hii kutokana na uchimbaji mchanga kwa ujenzi wa kupanua sehemu ya bandari ya Mombasa.

Utafiti uliofanywa kutathmini athari za kijamii na za kiuchumi kutokana na shughuli hiyo unasimulia jinsi sekta ya uvuvi katika maeneo husika ilivyo sambaratishwa. Kwa mujibi wa ripoti hiyo, mapato ya wavuvi kaunti za Kwale na Mombasa yameporomoka mno kutokana na upungufu wa samaki baharini.

“Makadirio ya mapato ya wanachama wa ufuo (BMU) wa Timbwani yameshuka kwa milioni 14.5, huu ukiwa ni upungufu wa asilimia 80 kwa mapato ya kila mwezi,” inaeleza ripoti hiyo iliyozinduliwa Ijumaa wiki iliyopita na shirika la wamiliki wa hoteli za kiutalii (KAHC).

BMU ya Timbwani iko Likoni katika eneo la ufuo wa Shelly ambapo imedaiwa kuwa uchafu uliochimbwa ili kuzidisha kimo cha maji bandarini umekuwa ukitupwa kwenye bahari ya Shelly.

Uchimbaji wa mchanga nao umesemekana kutekelezwa kwenye fuo za bahari ya Tiwi na Waa kaunti ya Kwale.

“Mapato ya mwaka mzima kwa baadhi ya wanachama wa BMU ya Tiwi yameporomoka kwa asilimia 95 na hili linaashiria kuwa wamepoteza takriban mapato yote walokuwa wakipata,” imedokezea ripoti hiyo.

BMU ndiyo kitengo cha msingi kabisa katika sekta ya uvuvi na kwa kawaida huwa kimewajumuisha wavuvi, wamiliki wa maboti, wanabiashara wa samaki pamoja na wadau wengine wanaotegemea fuo za bahari kama kitego uchumi.

Uchimbaji huo wa mchanga wa baharini umekuwa ukifanywa na meli inayojulikana kama Willem van Oranje. Kulingana na ripoti hiyo, shughuli yenyewe inahusisha kutumia presha kunyonya mchanga uliopo sakafuni mwa bahari hivyo basi kuwa chanzo cha uharibifu mkubwa ambapo viwango vya uzalishaji wa samaki vimepungua.

Upungufu huo umeathiri viwango vya uvuvi na hatimaye kusambaratisha mapato ya wavuvi. Wavuvi walokuwa wanapata zaidi ya kilo 100 za samaki kila siku huko Tiwi wameripotiwa kutopata chochote katika kipindi ambacho uchimbaji mchanga umekuwa ukiendelea.

Katika ufuo wa Shelly huko Likoni, watu walokuwa wakivua hadi kilo 50 kwa siku nao wameripotiwa kupata hadi kilo tano pekee wakati utupaji wa uchafu umekuwa ukifanyika. Isitoshe uchafuzi huo wa mazingira ya baharini pia umesemekana kuwa chanzo cha aina mbalimbali za samaki kupungua, kutokana na uharibifu wa sehemu za samaki kuzaana.

“Wavuvi wa pweza wameeleza kuwa kuna nyakati wameshindwa kufanya uvuvi kwa muda wa wiki mbili kwa sababu pweza wamekuwa vigumu kupatikana,” inasema ripoti. “Wengine wameripoti kwamba mapato yao yameshuka kutoka takriban shilingi 15,000 kwa siku kwa watu sita hadi kufi kia Sh1000 ama 2000 kwa siku. Wengine nao wamesema kwamba mapato yao yamekuwa chini ya shilingi 300,” imeongezea kusema. Zidisha utegemeaji wa samaki wa kutoka nje hususan samaki wa Uchina.


Read More

Feedback