Duale apinga mchango wa Shirika la Msalaba Mwekundu

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa  Aden duale,  amekoa vikali wito wa mchango kwa walioathirika na ukame uliotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu kwa Wakenya.  Duale amesema Shirika hilo linastahili kueleza kwa kina matumizi ya  fedha zilizochangwa wakati kulikuwa na ukame miaka minane iliyopita.

Akizungumza katika Chuo cha mafunzo ya Walimu cha Garissa,  Duale ametoa wito kwa Wakenya kutochanga. Amedai kuwa Shirika hilo linatumia janga la njaa kuwalaghai Wakenya.

Vilevile Kiongozi huyo amedai kuwa Shirika hilo lilipewa shilingi bilioni 1 na serikali mwaka jana kuwajengea makazi walioathirika na mafuriko katika maeneo ya Budalang'i, Tana River, Garissa na Meru, ilhali hadi sasa hakuna kilichotekelezwa. Sasa anaitaka serikali ichunguze jinsi fedha hizo  zilitumika.

Aidha, Duale awakashifu vikali viongozi wa maeneo ya  Turkana, Baringo, Wajir, Tana River, Garissa, Isiolo na  Marsabit kwa kutowajibika vilivyo katika kupigana na janga la njaa, akisema kuwa Kaunti hizo ni miongoni mwa zile   zinazotengewa kiasi kikubwa cha fedha na serikali kuu, Turkana ikongoza na shilingi bilioni 11.

Ikumbukwe siku ya Alhamisi wiki iliyopita, Shirika la Msalaba Mwekundu lilitoa wito kwa Wakenya kuchanga takribani shilingi milioni laki nane zitakazowasaidia Wakenya milioni 1.1  walioathirika na ukame, huku Katibu Mkuu wa Shirika hilo Abass Gullet ,akisema kuwa Kaunti za Turkana, Baringo na Wajir zimeathirika pakubwa.

Related Topics