''Caroline Mwatha alifariki alipojaribu kuavya mimba'' imesema ripoti ya upasuaji

Mwanaharakati Caroline Mwatha alifariki baada ya kutokwa damu kupita kiasi alipojaribu kuavya mimba. Daktari Peter Muriuki Ndegwa aliyeiwakilisha familia yake, amesema marehemu Caoline alikuwa na ujauzito wa kati ya miezi mitano na sita. Upasuaji uliofanyiwa mwili wake katika Hifadhi ya Maiti ya Umash , Nairobi umethibitisha hilo na kubainisha kuwa kijusi cha kiume kilikuwa bado kwenye uterasi. Pia uterasi wenyewe uliharibiwa vibaya, na kusababisha damu nyingi kuingia kwenye tumbo. Aidha mpasuaji huyo alisema kichwa cha kijusi hicho kilikuwa kimejeruhiwa kidogo, na mwili wake ulikuwa rangi ya kijivu, ishara ya kupoteza damu nyingi.

Wakati uo huo, dakatari Ndegwa amesema Marehemu hakuwa na majeraha yoyote ila yale ya sindano hivyo kufutilia mbali madai kuwa huenda alidhulumiwa kabla ya kifo chake. Ndegwa alisema uchunguzi zaidi utafanywa ili kubaini dawa iliyotumika kufanikisha shughuli hiyo.

Hata hivyo amesema hawakubaini iwapo Caroline alitekeleza uaviaji mimba huo kwa ihari au huenda alilazimishwa na kupendekeza uchunguzi zaidi kufanywa na idara za usalama.

Upasuaji wenyewe ulishuhudiwa na madaktari kadhaa wanaoiwakilisha familia ya Caroline, maafisa wa Shirika la Kutetea Haki za Kijamii la Dandora na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Haki Afrika ambayo yamesisitiza kuwa haki sharti itendeke.

Ripoti hiyo ya upasuaji inayathibitisha madai ya Idara ya Upelezi DCI yaliyotolewa Jumanne wiki hii kwamba Caroline alifariki dunia alipokuwa akijaribu kuavya mimba. Mkuu wa idara hiyo George Kinoti alisema uavyaji huo ulifaywa katika Kliniki ya New Njiru na daktari kwa jina Michael Onchiri na mmiliki wa kliniki yenyewe Betty Akinyi.

Maafisa wa upelelezi wanaamini kwamba Caroline alifariki katika hospitali hiyo na mwili wake kupelekwa katika hifadhi ya City tarehe 7 alfajiri sa kumi na dakika 42. 

Related Topics

Caroline Mwatha