Matokeo ya KCSE yatangazwa:
Na Carren Omae
Kwa mara nyingine, Waziri wa Elimu, Dkt. Fred Matiang'i, ametangaza matokeo ya mtihani wa kitaifa mapema mno tofauti na miaka ya awali, tena kwa kushtukizia - bila ufahamu wa wengi kuwa yangetangazwa . Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne, KCSE mwaka huu yametangaza, siku nne tu baada ya usahihishaji kukamilika Jumamosi iliyopita.
Katika matokeo hayo, ni watahiniwa elfu sabini na sabini na watatu pekee miongoni mwa watahiniwa wote laki sita, elfu kumi na tano, mia saba sabini na watatu, ndio waliopata grezi za C+ na zaidi, za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu vya umma chini ya ufadhili wa serikali. Idadi hii imepungua kutoka watahiniwa elfu themanini na wanane mia tisa ishirini na tisa wa mwaka jana. Aidha, Matiang'i amesema idadi ya watahiniwa waliopata gredi ya A imeongezeka kwa mwanafunzi mmoja pekee kutoka watahiniwa mia moja arubaini na mmoja mwaka huu hadi mia moja arubaini na wawili mwaka uliotangulia. Vilevile idadi ya waliopata gredi za A- imepungua kutoka watahiniwa elfu nne mia sita arubaini na watano hadi elfu mbili mia saba na kumi na watano mwaka huu.
Hata hivyo, ametangaza kuwa watahiniwa waliofanya bora katika masomo kumi na matatu mwaka huu yakiwamo Hisabati, Kiingereza na Jiografikia katika kulinganisha na mwaka jana. Vilevile watahiniwa wa kike wamefanya bora kuwazidi wenzao wa kiume, huku shule za wasichana pia zikiimarika zaidi mwaka huu. Waziri Matiang'i amezitaja Shule ya Wasichana ya Kenya High na Alliance kuwa zilizotia fora huku matokeo ya Shule ya Wasichana ya Pangani yakiimarika zaidi.
Kuhusu udanganyifu katika mitihani, Waziri Matiang'i amesema jumla ya shule kumi zinachunguzwa kwa madai ya kushiriki udanganyifu. Amesema matokeo ya shule hizo yatatangazwa punde uchunguzi utakapokamilika na ripoti kutolewa. Ripoti hiyo itatolewa Januari tarehe 18.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Huduma za Walimu, TSC Nancy Macharia alisema wamepokea orodha ya majina arubaini ya walimu wanaohusishwa na udanganyifu. Machari anasema uchunguzi unaendelea na iwapo watapatikana na hatia wataadhibiwa, kukiwamo kufutwa kazi huku akizionya shule za binafsi dhidi ya kuwaajiri walimu ambao wamefutwa kazi na TSC.
Haya yanajiri wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta ameiagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, kufanya uchunguzi wa kuhakikisha walimu mia saba wanaotuhumiwa kushiriki udanganyifu tangu mwaka 2017 wanaadhibiwa.
Akizungumza wakati wa kutangazwa kwa matokeo hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani KNEC, George Magoha amewaonya wanaopinga mpango wa kutathimini utendakazi wa walimu.
Watahiniwa wa KCSE waliufanya mtihani wao kati ta tarehe 6 Novemba na 29 huku usahihishaji ukifanyika kati ya Novemba 11 na Desemba 16. Ili kubaini kuhusu matokeo, tuma arafa yenye nambari ya usajili ya mtahiniwa kwa nambari 22252.