Igathe ataka picha za Kidero ziondolewe ofisini

Na, Beatrice Maganga
Igathe ataka picha za Kidero ziondolewe ofisini
Makali ya magavana na manaibu wao yameanza kudhihirika huku kisanga kikishuhudiwa leo katika ofisi za Kaunti ya Nairobi wakati Naibu Gavana wa kaunti hii, Polycarp Igathe alipozuru ghafla ofisi za kaunti hiyo na kuwaagiza wafanyakazi kuziondoa picha za aliyekuwa Gavana, Evans Kidero zilizokuwa zingali ukutani. Igathe amewakaripia wafanyakazi hao huku akitaka kupewa maelezo kuhusu suala la kusalia kwa picha hizo ilhali kuna gavana mpya ambaye ni Mike Mbuvi Sonko.
Igathe amesema kutoziondoa picha hizo za Kidero ni ukiukaji wa katiba ikizingatiwa kuwa kuna gavana mpya. Sonko aliapishwa Jumatatu wiki hii kuchukua hatamu za uongozi katika hafla iliyoandaliwa kwenye Bustani ya Uhuru na kuhudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Kidero na viongozi wengineo.
Hata kabla ya kuapishwa rasmi, gavana mpya wa Nairobi alimtaka Kidero kutozichukua fedha zozote kutoka akaunti za benki za kaunti. Mojawapo la mabadiliko ambayo utawala mpya wa serikali ya Nairobi umeaza kutekeleza ni kukabili tatizo la ukosefu wa maji na kuahidi kuboresha huduma za matibabu na mpango bora wa uzoaji taka.
Hayo yanajiri huku Kaunti ya Kiambu ikiwa ya hivi punde kuwapa likizo ya lazima maafisa wake wa ngazi za juu na kuagiza utendakazi wao kuchunguzwa.
Maafisa wa utawala wa Wadi sitini na maafisa wa mawasiliano wamepokezwa barua za agizo hilo mapema leo. Maafisa wa mawasiliano wamepewa likizo ya siku thelathini iliyoanza jana huku wakitakiwa kurejesha magari na vifaa vyote vya kaunti kwa wakuu wao. Likizo hiyo inatazamiwa kukamilika Oktoba tatu ambapo watafahamishwa iwapo watarejea kazini au la.
Hapo jana, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi alichukua hatua sawa na hiyo na kuamuru uchunguzi wa wafanyakazi na matumizi ya fedha kwenye kaunti hiyo. Kaunti nyingine ambazo zimechukua hatua mbalimbali dhidi ya wafanyakazi wake ni Machakos, Busia, Siaya, Tharaka Nithi miongoni mwa nyingine. Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Umma, PSC, Margaret Kobia, amewaonya magavana kuhusu hatua wanazochukua dhidi ya maafisa wa kauti akisema sharri sheria izingatiwe.

Related Topics