KDF wawaokoa watu sita akiwamo katibu waliotekwa nyara: Na Beatrice Maganga
Maafisa wa Jeshi la KDF kwa ushirikiano wa polisi wa kitengo cha GSU wamefaulu kuwaokoka watu sita akiwamo Katibu wa Wizara ya Ardhi na Nyumba, Mariam Elmawy waliotekwa nyara na washulikiwa wa Al Shabaab eneo la Lamu. Sita hao walikuwa wametekwa katika eneo la Milihoi na kuelekezwa katika Msitu wa Boni.Katibu huyo alikuwa akielekea eneo la Witu kuzitembelea familia zilizoyahama makwao kufuatia ukosefu wa usalama baada ya kuhudhuria mkutano na washikadau wanaoendeleza ujenzi wa mradi wa Lapset.
Magari mawili ambayo awali yalitekwa yameachiliwa huru. Inadaiwa kwamba washukiwa wa Al Shabaab takriban thelathini wamehusika katika utekaji huo. Awali mhudumu mmoja wa lori alitekwa katika eneo lilo hilo na kuelekezwa Msitu wa Boni huku dereva akiruhusiwa kuendelea na safari.
Tukio hili linajiri wakati maafisa wa usalama wanaendeleza oparesheni katika msitu wa Boni kuwasaka washukiwa wa Al Shabaab ambao siku chache zilizopita waliwaua watu tisa maeneo ya Jima na Pandanguo. Ni hivi majuzi ambapo polisi watatu waliuliwa eneo hilo.
Wikendi iliyopita Kaimu Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i alitoa marufuku ya kutotoka nje kati ya saa kumi na mbili unusu jioni na saa kumi na mbili unusu asubuhi kwa wakazi wa maeneo ya kaunti za Lamu, Tana River na Garissa kwa kipindi cha miezi mitatu kufuatia kukithiri kwa visa vya utovu wa usalama.