×
App Icon
The Standard e-Paper
Home To Bold Columnists
★★★★ - on Play Store
Download Now

KHRC yasema deni la umma la wanyanyasa wakenya

Mwana biashara wa mali reja reja asukuma mkokoteni kwenye barabara kuu ya Mombasa Juni 12, 2025. [Elvis Ogina, Standard]

Mwelekeo wa sasa wa kiuchumi wa Kenya unaondoa rasilimali kutoka kwa huduma muhimu na kuzidisha ukosefu wa usawa kwa umma.

Kulingana na ripoti ya tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) hali hii inazidisha dhuluma za kihistoria, haswa zile zinazohusiana na ardhi.

Ripoti ya kwanza, ‘Uchumi wa Ukandamizaji’, inaonesha kwamba fedha za umma za Kenya sasa zimepangwa kwa njia zinazowadhuru watu wa kawaida.

Kulingana na KHRC, asilimia 68 ya mapato yote ya kawaida hutumika kulipa deni la umma na mishahara ya serikali, na kuacha chini ya theluthi moja ya bajeti ya afya, elimu, usalama wa chakula, maji, usafi wa mazingira, nyumba, na ulinzi wa kijamii.


Ripoti hiyo inafuatilia jinsi mgogoro huu ulivyokuwa; katika miaka minne tu, riba ya deni la umma imeongezeka hadi asilimia 25 kutoka asilimia 18 ya matumizi yote, na hivyo kupunguza pesa kutoka kwa huduma muhimu.

Mipango iliyolenga kuwalinda raia walio katika mazingira magumu imepungua hasa inapohitajika zaidi; hii ikiwa ni kulingana na ripoti hiyo.

Kwa mfano, usaidizi kwa wazee umepungua hadi shilingi bilioni 15 kutoka shilingi bilioni 18, ufadhili kwa yatima umepungua hadi shilingi bilioni 5 kutoka shilingi bilioni 7, huku rasilimali kwa watu wenye ulemavu zinaendelea kupungua katika hali halisi.

Sekta ya afya pia imeathiriwa pakubwa; katika Kaunti ya Nairobi pekee, matumizi halisi ya afya yameshuka hadi shilingi bilioni 7 kutoka shilingi bilioni 8, licha ya idadi ya wakazi zaidi ya milioni 5.7 wanaoishi katika Kaunti hiyo.

Wakati huo huo, miswada inayosubiriwa ya kaunti imeongezeka, sasa ikiwa mara 300 zaidi ya matumizi yote ya kaunti, miswada ya mishahara ikitumia karibu nusu ya bajeti nzima, na kuacha kidogo sana kwa huduma ambazo raia hutegemea.

Kulingana na ripoti hiyo, matumizi haya mabaya ya kifedha yana matokeo yenye uchungu hasa kwa umma.

Familia ziliiambia KHRC kuhusu hospitali zisizo na dawa, wagonjwa kuzuiwa kupata matibabu kwa kukosa bima, na masomo ya shule kutatizwa kwa sababu serikali ya kitaifa inachelewesha kutuma fedha za ruzuku.

Vijana waliripoti kupoteza kazi huku biashara zikipambana na kodi isiyokoma.

Watu wenye ulemavu wanasubiri kwa miaka mingi kupata msaada, huku akina mama wasio na waume na familia katika makazi yasiyo rasmi wakisema wametengwa kabisa.

Ripoti ya pili, iliyopewa jina “Nani Anamiliki Kenya? yaani kwa kimombo, ““Who Owns Kenya?”, inaonesha kwamba mgogoro wa kiuchumi wa Kenya pia unatokana na ukosefu wa usawa wa ardhi.

Kwa mujibu wa KHRC, ardhi inasalia kuwa rasilimali muhimu zaidi nchini, lakini umiliki wake hauna usawa, kwani chini ya asilimia mbili ya Wakenya wanamiliki zaidi ya nusu ya ardhi ya kilimo nchini, sehemu kubwa ikiwa imebaki bila shughuli au kupatikana isivyo halali.

Wakati uo huo, asilimia 98 ya mashamba yote, mengi yakiwa madogo na ya wastani wa hekta 1.2 pekee, yanamiliki asilimia 46 pekee ya ardhi inayolimwa, huku asilimia 0.1 ya wamiliki wa ardhi wakubwa wakimiliki asilimia 39.

Ripoti inasema umiliki huu unawanyima mamilioni ya Wakenya fursa ya kupata riziki, kwani unapunguza uzalishaji wa kilimo, unachochea ukosefu wa usalama wa chakula, na unawafungia vijana na wanawake fursa za kujipatia utajiri.

Pia inahusishwa na mgogoro wa njaa unaoendelea nchini Kenya, ambapo watu milioni 2.2 kwa sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku Kenya ikipata alama 25 kwenye Fahirisi ya Njaa ya Dunia, na kuiweka katika kundi la "hali mbaya zaidi".

Ripoti inaonyesha kwamba ardhi ya jamii bado iko katika hatari kubwa ya unyakuzi.

Ucheleweshaji wa usajili, hati miliki bandia, udanganyifu wa mipaka, na uhamishaji wa watu uliochochewa kisiasa unaendelea kuhamisha jamii.

Mfano, katika ukanda wa Pwani, zaidi ya asilimia 65 ya wakazi katika kaunti kama vile Kilifi, Kwale, na Lamu hawana hati rasmi za ardhi, na hivyo kuacha vizazi kusalia kuwa masqwota kwenye ardhi ya mababu.

Kaunti hizi pia ni ambazo hupata alama chini ya wastani wa kitaifa katika afya, elimu, na mapato.

Hata hivyo, licha ya thamani kubwa ya kiuchumi ya ardhi, kodi zinazotokana na ardhi huchangia chini ya asilimia moja ya mapato yote ya kaunti katika kaunti nyingi.

Wamiliki wa ardhi wakubwa wanaendelea kunufaika na kodi hafifu wanazotozwa, orodha za tathmini zilizopitwa na wakati, kuingiliwa kisiasa, na tathmini ya kimakusudi ya thamani ya mali.

Baadhi ya maeneo yenye thamani kubwa, kama vile Karen na Muthaiga jijini Nairobi, na Diani, Mtwapa, na Watamu katika eneo la Pwani, yamekuwa yakipuuzwa kwa miongo kadhaa, na hivyo kuruhusu matajiri kulipa kodi kidogo sana kuliko wanavyopaswa kulipa.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Kenya inaendesha mifumo miwili ya kiuchumi: mmoja kwa matajiri, wanaofurahia upatikanaji wa ardhi, ulinzi wa kisiasa, na kodi ndogo, na mwingine kwa raia wa kawaida, ambao hulipa kodi kubwa kwa bidhaa na mapato ya msingi huku wakipokea huduma chache za umma.

Licha ya haya, ripoti hiyo pia inasema kwamba ardhi inasalia kuwa kitovu cha suluhisho.

Kuanzisha kodi imara na inayoendelea ya thamani ya ardhi kunaweza kubadilisha mfumo wa mapato wa taifa la Kenya.

Kutoza kodi ardhi isiyo tumiwa na ya kubahatisha kunaweza kupunguza ulimbikizaji wa ardhi, kupunguza bei, kukuza matumizi ya ardhi yenye tija, na kufungua rasilimali kwa kaunti.

Mfumo wa kodi ya ardhi uliotekelezwa vizuri unaweza kuongeza mapato makubwa; makadirio yanaonesha kuwa kodi ya utajiri nchini Kenya inaweza kuzalisha hadi shilingi bilioni 125, karibu mara mbili ya bajeti ya sasa ya ulinzi wa kijamii.

KHRC inatoa wito kwa utawala wa Rais William Ruto kufikiria upya jinsi nchi inavyokusanya na kutumia rasilimali zake.

"Kenya inahitaji maamuzi ya kiuchumi yanayowaweka watu mbele, kulinda haki, na kuhakikisha usambazaji wa haki wa rasilimali za kitaifa," mkurugenzi mtendaji wa KHRC Davis Malombe alisema wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Davis Malombe ameongeza kwamba, "Hii ni pamoja na kupunguza upotevu na ufisadi, kusimamia deni kwa uwajibikaji, kuimarisha uwazi, kurekebisha kodi ya ardhi, na kusaidia jamii ambazo zimepuuzwa au kuhamishwa."