Hali ya taharuki inaendelea kutanda katika eneo la Mishomoroni kwenye Kaunti ya Mombasa kufuatia kuuliwa kwa wanachama watano wa genge la vijana lililotekeleza uvamizi kwenye baadhi ya mitaa ya eneo hilo jana jioni.
Wenyeji wanahofia usalama wao huku wakihisi kwamba huenda wanachama hao wakalipiza kisasi baada ya mazishi ya watano hao.
Baadhi ya wenyeji ambao tumewahoji wamekiri kuwatambua baadhi ya wanachama ambao wamekuwa wakiwahangaisha mara kwa mara wakisema hujificha katika mtaa wa Junda.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kisauni Julius Kiragu amesema kwamba mafisa zaidi wametumwa kushika doria eneo katika hilo ili kuhakikisha usalama unadumishwa.
Jana mwendo wa saa kumi na moja jioni genge la zaidi ya wanachama thelathini waliokuwa wamejihami kwa panga na visu waliwavamia wakazi wa mitaa tofauti tofauti ya Mishomoroni.
Kulingana na walioshuhudia, wanachama hao walianza kuuvamia mtaa wa New Hope kisha Kasarani, Calvary, Kadzonzo na hatimaye mtaa wa Milango Saba huku wakimkata yeyote waliyekutana naye.
Radio Maisha imebaini kwamba takriban watu kumi na mmoja walijeruhiwa kufuatia uvamizi huo. Tayari baadhi ya majeruhiwa walitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani huku wengine wakiendelea kutibiwa kwenye hospitali mbalimbali.
Genge hilo lilitekeleza uvamizi huo muda mfupi baada ya mazishi ya mwenzao aliyekuwa ameuliwa na umma usiku wa kuamkia jana.