21st September, 2018
Gavana wa kaunti ya Migori Okoth Obado amehojiwa katika makao makuu ya idara ya upelelezi hapa jijini Nairobi, kuhusiana na kifo cha Sharon Otieno.
Obado alijiwasilisha katika afisi hizo mapema hii leo baada ya kupokea mwito. Haya yanajiri siku moja baada ya matokeo ya vinasaba yaani DNA kubainisha kuwa ujauzito wa Sharon ulikuwa wa Obado.
Sharon alikuwa na uja uzito wa miezi saba alipokumbana na mauti yake. Hii ni mara ya pili kuhojiwa kwa gavana huyo.
Ikumbukwe msaidizi wa Gavana Obado Michael Oyamo na aliyekuwa mwakilishi wa wadi wa Kanyadoto Lawrence Mula ni miongoni mwa washukiwa wakuu wa mauaji hayo, wanaendelea kuzuiliwa.
Mwili wa Sharon ulipatikana tarehe tano mwezi huu.