Jicho Pevu: Dugudwa la Uchaguzi, Makala ya Kwanza

Jicho Pevu | Sunday 20 Apr 2014 12:00 am
Hayawi hayawi hatimaye huwa. Siku iliyokuwa ikisubiriwa na Wakenya hatimaye imetimia. Katika makala ya JICHO PEVU hii leo tunaangazia siri za ndani pamoja na uchaguzi tata wa mwaka uliopita. Mwanahabari wetu mpekuzi MOHAMMED ALI alifanikiwa kupata mawasiliano ya siri baina ya mshirika wa chama cha CORD na afisa mmoja mkuu wa IEBC na yaliyokuwa ya kupasua moyo kando na madai ya jamaa fulani kutoka ujasusi kuhusishwa kupenyeza hifadhi kuu ya kidijitali ya IEBC kutoa matokeo tofauti. Kando na hayo madai ya kudukuza kwa lugha ya kimombo ‘computer hacking’ pamoja na utumizi wa hifadhi hio yaani ‘server’ moja na kusambaratika kwa mashine ya kunasa jiometria ya mpiga kura ni miongoni mwa maswali tete ambayo tunauliza. Uchaguzi umepitwa na wakati lakini taarifa hii ni ya kutoa ukweli na kuangalia ni wapi tulipokwenda kombo kwa lengo la kuboresha na kuleta mabadiliko makhsusi na demokrasia halisi katika siku za usoni kama inavyopendekezwa na katiba inayomlinda kila mkenya.