19th February, 2021
Serikali imetoa tahadhari kwa wakenya walioajiriwa kupitia vyeti ghushi vya elimu kuwa wataandamwa na kukabiliwa kwa mujibu wa sheria. Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya taifa ya kutathmini na kuainisha hitimu, KNQA, dkt Juma Mukhwana, amesema tayari mamlaka hiyo imeishirikisha idara ya ujasusi, DCI, tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka, IEBC, na ile ya maadili na kupambana na ufisadi, EACC, ili kuwanasa wahusika. Aidha dkt mukhwana ameonya kwamba huenda watakaopatikana na hatia wakashtakiwa na kuagizwa warejeshe mishahara yote waliyopokea walipokuwa kwenye ajira.