Je, ‘Baba’ asalie tu kuwa mpishi na asile? Je, ni zamu ya ‘Baba’ kusema fulani tosha? Picha: Hisani

Wanasema watu “ukichelewa jamvini utakula Mende badala ya tende!” Msemo huu watokana na kasheshe, timbugo na hamna hamana za hamrere hamrere katika muungano wa Cord; muungano ambao kwamba ndio rasmi wa upinzani nchini Kenya.

Upinzani hapa kwa maana ya kuipeleka mchakamchaka serikali ya Jubilee inayoongozwa na rais Uhuru Kenyatta ili asipate deodeo la usingizi. Wasemavyo watu huko visiwani Zanzibar, kuizundua kutoka katika zuguzugu la usingizi!

Gumzo langu leo hii ni kuuhusu muungano huo wa Cord ni kukihusu chama mojawapo wa vyama vinavyounda muungano huo: ODM. Je, aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Mheshimiwa Raila Amollo Odinga anagutuka usingizini kukiwa kumekwisha kupambazuka au ni nini? Ama ndio mwanzo anatafuta blanketi wakati kumekucha? Hivi najaribu kusema nini leo? Tuache kwa muda hekaye hizo za kuchelewa mkekani na kula mende wakati walaji washatimka na tende.

Nakumbuka vizuri sana ni kama tu jana. Mwaka 2007. ODM ilikuwa ODM. Kote nchini. Pembe zote za jamhuri. Huo ulikuwa mwaka 2007. Nakumbuka vizuri chungwa lilivyoliwa kote nchini.

Tuache kisogo cha 2007. Tuje mbele. Kipaji sasa cha mwaka 2016, tukijongea uchaguzi mkuu mwakani, 2017. Ziara ya Agwambo magharibi ya Kenya baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa ODM mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba ‘kutimka’. ‘Baba’ amepokelewa kwa hisia mseto. Kikubwa yakiwa mabango katika kaunti ya Vihiga yaliyomuomba ‘arejeshe mkono’ kwa mwanasiasa aliyewahi kuwa makamu wa rais, wa muda mfupi zaidi nchini, Wycliffe Musalia Mudavadi.

Budalangi kwa aliyekuwa katibu mkuu wa ODM Ababu Namwamba kulikuwa na mapokezi ya raha na karaha. Kisha ilibidi ‘Baba’ kukwepa eneo la Mumias. Kisa na maana kulikuwa na tafrani ya vijana wakiwa na malalamishi mengi yakiwemo usimamizi ‘uliosambaratisha’ kampuni ya sukari ya Mumias. Siamini kuwa hawa ndio wakazi wa Mumias waliokuwa tayari kujitoa mhanga na kafara ili ‘Baba’ aingie ikulu 2007!

‘Baba’ amefanya ziara majuzi magharibi ya nchi. Aliandamana na jeshi kubwa tu. Ingawa kigogo wa siasa wa eneo hilo seneta wa Bungoma mheshimiwa Moses Masika Wetangula ‘analia’ kuwa hakujumuishwa kwenye msafara huo. Ewe!

Siku hiyo ya kilio cha kutojumuishwa safarini, mheshimiwa Wetangula akinukuliwa kwenye runinga ya KTN, aliweka bayana kuwa imefika zamu ya ‘Baba; kuachia ngazi na kumuunga mkono mgombea mwengine wa urais. Usisahau kuwa mbali na ‘Baba’, wagombeaji wengine wa urais, kwa sasa, katika mrengo wa Cord ni pamoja na Moses Wetangula na mwenyekiti wa chama cha Wiper Mheshimiwa Stephen Kalonzo Musyoka.

Huku Weta akijipigia debe na kutoa kauli hiyo ya majuzi, imeendana na kauli aliyowahi kuitoa siku si nyingi seneta wa Mombasa rafiki yangu Hassan Omar Sirai akimwomba ‘Baba’ amuunge mkono Bw. Kalonzo. Mheshimiwa Omar kachaguliwa useneta kwa tiketi ya chama cha Wiper katika muungano wa Cord. Kila mwamba ngoma...

Pwani iliyokuwa ngome ya ODM siku si nyingi zilizopita, sasa ina madoadoa. Hali imebadilika pakubwa ‘Baba’! Je, ‘Baba’ ageuke na kuwa Lionnel Andres “Leo”Messi? Yaani Messi kashinda kila taji akiwa Barcelona, lakini timu ya taifa ya Argentina, ng’o! Imebidi astaafu kuichezea timu ya taifa. Japo nina imani ataghairi. Je, ‘Baba’ asalie tu kuwa mpishi na asile? Je, ni zamu tena ya ‘Baba’ kusema....tosha?