Mawakili wa Seneta wa Nairobi Jonson Sakaja wamepuuza hoja kwamba picha za sherehe ya kufuzu kwa Sakaja, zinafaa kutolewa ili kutumika kuthibitisha uhalali wa digrii yake.

Aidha, upande wa utetezi umesema si lazima kwa Sakaja kutoa stakabadhi zote za kubainisha iwapo alisoma mwaka wa 2017 katika Chuo Kikuu cha Team nchini Uganda ama la, na kwamba ni porojo kwa yeyote kupinga uhalali wa digri yake kwa msingi huo.

Sakaja kupitia mawakili wake, akiwamo Elias Mutuma, amepongeza uamuzi wa Kamati ya Kusuluhisha Mizozo katika Tume ya Uchaguzi IEBC, wa kumwidhinisha kuwania ugavana kupitia chama cha UDA

Aidha, Wakili Mutuma amekosoa ushahidi wa upande wa mlalamishi kupinga ugombea wa Sakaja, akisema ushahidi huo unajumuisha maneno ya kusikia tu bila uhakika.

Jaji Anthony Mrima wa Mahakama Kuu ya Milimani ameanza kusikiza kesi hiyo Jumatatu, ambayo iliwasilishwa na mlalamishi Dennis Wahome, anayeshinikiza Tume ya Uchaguzi IEBC kutochapisha jina la Seneta Sakaja katika karatasi za kupigia kura.

Wahome kupitia Wakili Njoki Mboce, anaitaka mahakama hiyo kutupilia mbali uamuzi wa IEBC kumwidhinisha Sakaja.

Alhamisi iliyopita, Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu ilibatilisha uhalali wa digrii ya Sakaja.