Na, Sarah Otieno/ Beatrice Maganga Viongozi wa muungano wa NASA wamelazimika kukatiza ziara zao mjini Kabarnet Kaunti ya Baringo baada ya kundi la vijana kuzua vurugu  walipokuwa wakihutubu. Kwa mujibu wa wakazi, ghasia hizo zilichangiwa pakubwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe 'Ruto shoot to kill' wakisema hali hiyo ilichangia taharuki. Vijana hao aidha wameteketeza  mabango na mashati-tao ya  NASA  na kuvalia yale ya chama cha Jubilee. Raila aliyezungumza baadaye aliikashifu serikali ya Jubilee akidai haijaangazia masuala ya usalama wa wakazi wa eneo hili, suala ambalo limesababisha vifo na wakazi kupoteza mali yao.   Kauli yake imesisitizwa na  Musalia Mudavadi na Gavana wa Bomet, Isaac Ruto ambao wamewashtumu vijana wanaokubali kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu katika mikutano ya kisiasa.   Ziara hiyo inajiri wakati idadi ya walioaga dunia kufuatia shambulio la wezi wa mifugo eneo la Mochongoi, Baringo Kusini imefikia watano baada ya mili miwili kupatikana leo katika Msitu wa Lomoiwe.