Na Beatrice Maganga Maafisa wanne wa polisi wanaohudumu katika Kituo cha Polisi cha Hamey kwenye mpaka wa Kenya na Somalia wameripotiwa kutoweka baada ya kituo chao kuvamiwa na washukiwa wa kundi gaidi la Al Shabaab. Washukiwa hao wameripotiwa kutoweka na bunduki kadhaa pamoja na gari la polisi wakati wa uvamizi huo uliotekelezwa usiku wa kuamkia leo. Maafisa wawili aidha walijeruhiwa vibaya kwenye kisa hicho na tayari wamesafirishwa kwa ndege hadi Nairobi kwa matibabu zaidi. Walioshuhudia kisa hicho wanasema wavamizi hao vilevile walitoweka na sare za polisi. Maafisa zaidi wametumwa katika kituo hicho huku doria ya angani na ardhini ikiimarishwa kuwasaka wahusika wanaoaminika kutoroka na kuingia Somalia.