Na, Sophia Chinyezi

Siku moja baada ya Kamati ya Pamoja kuhusu IEBC kuwasilisha ripoti yake kwa mabunge ya Seneti na Taifa, viongozi mbalimbali wameendelea kutoa kauli zao kuhusu maafikiano ya jinsi makamishna wa IEBC wataondoka ofisini. Mashirika ya kijamii yanataka makamishna wa Tume ya Uchaguzi IEBC kushtakiwa, yakisema hawastahili kuondoka ofisini kwa heshima kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Pamoja iliyokuwa ikishughulikia marekebisho kwenye tume hiyo. Wanasema kila kamishna anafaa kuwajibika na kwamba maafikiano kati yao na kamati hiyo yanakiuka katiba. Mashirika hayo chini ya mwavuli wa 'Kura Yangu, Sauti Yangu,' vile vile yamepuuza pendekezo la kamati hiyo la kuwapo kwa jopo litakalowahusisha wakuu wa mashirika ya dini kuendesha shughuli ya kuwateua wakuu wapya wa IEBC.   Ikumbukwe ripoti ya kamati hiyo kuhusu IEBC iliwasilishwa bungeni jana ambapo itajadiliwa wiki ijayo. 'Kura Yangu, Sauti Yangu,' ina wawakilishi kutoka Tume ya Kutetea Haki za Binadamu KHRC, IMLU, Inuka Trust miongoni mwa mashirika mengine. Wameyasema hayo katika ofisi za KHRC jijini Nairobi.  

 


IEBC;KHRC;IMLU