Na, Carren Omae

Idara ya Magereza imewaachisha kazi kwa muda maafisa wanane kufuatia kisa ambapo wafungwa wanne walitoroka kutoka gereza la Kibos Mjini Kisumu. Miongoni mwa waliofutwa kazi kufuatia uchunguzi wa awali ni afisa aliyekuwa kazini kisa hicho kilipotokea. Kamanda wa Idara ya Magereza eneo la Nyanza, Amos Misik amesema maafisa hao wameachishwa kazi ili kutoa nafasi ya uchunguzi kufanywa. Hayo yanajiri huku polisi mjini humo wakiendelea kuwasaka wafungwa hao. Mkuu wa Polisi eneo hilo, Joseph Keitany amesema wanne hao walikuwa wakizuiliwa kwa tuhuma mbalimbali na kwamba msako dhidi yao unaendelea. Waliotoroka ni Douglas Onyancha, ambaye vilevile anakabiliwa na mashtaka ya Kumuua mfungwa mwenzake katika gereza la Kodiaga. Wengine ni Kennedy Wesonga, Keneth Lekesho na Salim Sifuna kwa jina jingine, Masibo.