Ilinibidi kuzima runinga yangu pale Kuria aliposema IEBC ni ya Raila Odinga  Picha: Hisani

Ni kweli kuwa maskini hana chake humu nchini.

Hivyo, amejitengea nafasi moja tu — ile ya ukiritimba na utumwa. Kazi yake imekuwa kupiga siasa za ukabila na kumwaga damu kwa niaba ya wahuni wakuu wanaojiita viongozi. Hata akifa maskini hamna anayeguswa, huku siasa zikichukua kipao mbele katika vifo vyao.

Hivi majuzi wakenya kadhaa walifarikikatika mkasa wa jumba la orofa huko katika mtaa wa Huruma. Kabila zote katika mtaa huo ziliungana pasi na Mjaluo, Mkikuyu, Kalenjin, Mkamba au Mluhya ili kusaidia kuwakomboa waliokuwa wamekwama ndani ya jumba hilo. Maskini walishirikiana kwa mapenzi ya hali ya juu usiku kutwa huku matajiri wakilala na kufanya mapenzi ya kuongeza utajiri zaidi majumbani mwao. Maskini walikaidi mvua usiku kucha ili kuwaokoa wenzao waliokwama.

Kulipopambazuka, waongo wa ukabila wanaojiita viongozi, waliamka na kupokea taarifa hizo. Lakini badala ya kutafuta suluhu, walifika mahali pale kila mmoja akitaka kujionyesha bora zaidi ya mwengine mbele ya kamera za wanahabari. Wengine waliweka mabango ya jina zao kufanya kampeni wakati huu wa shida. Wengine walianza kulaumiana. Viongozi wa dini nao hawakuwachwa nyuma katika mchezo huu wa kisiasa.

Rais Uhuru Kenyatta naye alikuwa akifanya kazi muhimu zaidi — ile ya kuchoma pembe za ndovu na kifaru. Kamwe hakusitisha shughuli hizo — kumbuka pembe hazina miguu, hivyo haziwezi zikatembea toka mahala pale.

Aliyesema kuwa ni heri kuzaliwa paka ulaya kuliko binadamu Kenya hakukosea.

Kabla ya mkasa huo, mama Lucy Kibaki, aliyekuwa mke wa rais wa Kenya wa tatu Mwai Kibaki, aliaga dunia kule Uingereza — Mungu ailaze roho yake pema. Habari za kifo chake viligonga vichwa vya habari huku vyombo vya habari vikikesha ili kupeperusha hari hiyo kwa wakenya.

Wakenya mtandaoni walijifanya mamoja na kumlimbikizia sifa kede kede huku wakisahau walivyomchukia na hata kumtusi miaka ya nyuma alipokuwa hai.

Siku tatu za kuomboleza kifo cha Mama Lucy ilitengwa. Huku wakenya wakiendelea kuombeleza kifo cha Mama Lucy, janga likawakumba maskini kule Huruma.

Lakini hamna mtu aliyewalimbikizia sifa watu hawa kwani ni maskini. Na ingawa wengi walikufa huku wengine wakipoteza mali yao, hakuna siku hata mmoja iliyotengwa kuomboleza na familia ya waathiriwa.

Hii ndio Kenya ya kizazi kipya. Kenya ya dharau na utumwa. Walipokufa wanajeshi wetu huko Somalia, katika mashambulizi ya kinyama El Adde, hata bendera haikushushwa nusu mlingoti kwa sababu waliokufa hawakuwa watoto wa matajiri. Hivi ni taifa gani duniani wanajeshi wake wanauawa kama mbwa na hata hamna heshima kwao?

Haya ndiyo maswali mazito tunaofaa tujiulize. Yafaa tufahamu kuwa sisi ndio serikali — sio wahuni wachache wanaotumaliza kila kukicha.

Nilitazama kwa hofu huku miili ya walokufa katika mkasa wa Huruma ikipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha maskini cha City. Hii ndio demokrasia ya maskini na tajiri. Maskini akifa ni ushuzi, tajiri akifa Kenya inasimama.

Tukio la vyumba kuporomoka sio geni Kenya. Lakini kila mara tunapokumbwa na janga kama hili, viongozi huto ahadi tele. Kinachofuatia huwa ni kumtia mbaroni mwenye jengo huku maafisa walioruhusu jengo kujengwa wakipigiwa makofi.

Siku mbili baada ya matukio haya ya kuuzunisha, nikiwa nimejituliza kwangu kama kasuku, niliwaona viongozi wakipiga siasa siku ya Leba Dei — tukio la Huruma lilzikwa katika kaburi la sahau, na kawme hawakutajwa.

Nlitazama huku viongozi kama vile Johnson Sakaja, Moses Kuria, Francis Atwoli na Mike Sonko wakicheza mchezo wa kisiasa iliyojaa uongo. Ilinibidi kuzima runinga yangu pale Kuria aliposema IEBC ni ya Raila Odinga. Huu ni upumbavu wa hali ya juu.

Watu hawa wanaojiita viongozi, huku kazi yao ikiwa ni kupiga siasa hata wakenya wanapoangamia ni watapeli.

Mungu ailaze nyoyo za waote waliokufa akiwemo Mama Lucy Kibaki mahala pema panapolazwa wema.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter:

@mohajichopevu