Na Beatrice Maganga Licha ya pingamizi zilizoibuliwa na wanasiasa dhidi yake, Laban Ayiro amechukua hatamu rasmi kuwa Kaimu Naibu Mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha Moi, kwenye hafla iliyofanyika katika bewa kuu mjini Eldoret. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ayiro ametoa wito wa ushirikiano miongoni mwa washikadau wa chuo hicho ili kukiboresha zaidi. Kwenye hotuba yake ya kuondoka ofisini, aliyekuwa Naibu Mkuu, Richard Mibey amemtakia kila la heri mrithi wake. Siku ya Jumanne, Hapo jana Magavana Jackson Mandago wa Uasin Gishu, Alex Tolgos wa Elgeyo Marakwet, wabunge James Bett wa Kesses na mwenzake wa Kapseret, Oscar Sudi miongoni mwa wengine walitaka kipindi cha kuhudumu cha Naibu Mkuu, Prof, Richard Mibey kuongezwa kwa wiki moja ili kutoa nafasi ya kumtangaza rasmi mrithi wake. Wanasiasa hao walitishia kusambaratisha hafla ya kufuzu kwa wanafunzi chuoni humo itakayofanyika kesho na Ijumaa iwapo malalamishi yao hayatazingatiwa. Wanasiasa hao wanataka mzaliwa wa eneo hilo, kupewa nafasi ya kukiongoza chuo hicho.